Taifa Stars yajiweka njia panda CHAN 2018

Friday July 21 2017

 

By Saddam Sadick,Thomas Ng'itu

Mwanza.Tanzania 'Taifa Stars' imeshindwa kutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani baada ya kukubali kulazimisha sare ya bao 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa kusaka kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani(Chan2018).

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ilishuhudiwa Stars wakicheza kwa kiwango kibovu kipindi cha kwanza tofauti na wapinzani wao Rwanda.

Rwanda ilikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Dominique Nshuti katika dakika ya 18 baada ya kutumia uzembe wa mabeki wa Taifa Stars walioshindwa kuokoa krosi ya chini iliyopita katikati yao na kumkuta mfungaji aliyekwamisha mpira wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Stars waliongeza mashambulizi na kufanikiwa kupata penalti baada ya Rucogoza Aimambe kuunawa mpira eneo la hatari na kuonyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Alier Michael kutoka Sudan.

Nahodha Himid Mao aliipatia Stars bao la kusawazisha baada ya kuukwamisha mpira wavuni kwa mkwaju wa penalti.

Katika mchezo huo, Stars ilishindwa kucheza kitimu kipindi cha kwanza huku safu ya ulinzi ikikatika kila mara na kuruhusu mashambulizi mengi golini kwake.

Dakika ya 15 Stars ilipata pigo baada ya beki wake wa kulia Shomari Kapombe kuumia na kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Boniface Maganga.

Kapombe alionekana akilia na kubembelezwa na Himid Mao kabla ya baadae kulala chini na watu wa huduma ya kwanza kumtoa nje moja kwa mojan hata hivyo aliendelea kuangua kilio hata alipokuwa benchi.

Dakika ya 32 Barnabe Mubumbyi wa Rwanda aliikosesha timu yake bao  baada ya shuti lake kupaa juu ya lango huku Stars wakikosa bao dakika ya 45 baada ya Boniface  Maganga kuachia shuti kali lililopanguliwa kistadi na kipa wa Rwanda  Ndayishimiye Eric.

Kipindi cha pili Taifa Stars walirejea kwa kasi na kulishambuliaji lango la Rwanda kama nyuki lakini hata hivyo umakini wa washambuliaji wa timu hiyo wakiongozwa na John Bocco uliwakosesha ushindi.

Dakika ya 50 wachezaji wa Rwanda walimvaa mwamuzi, Alier Michael  wakidai penalti baada ya Salim Mbonde kuunawa mpira eneno la hatari  hata hivyo mwamuzi alimuru kuwa ni upigwe mpira wa faulo.

Katika mchezo huo wachezaji wawili wa Rwanda, kipa  Ndayishimiye na Bizimana Jihad walionyeshwa kadi za njano kwa kupoteza muda.