TPDC CUP kutimua vumbi Mtwara

Mtwara. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC limezindua mashindano ya mpira wa miguu, yatakayofahamika kama ‘TPDC CUP’ yanayoshirikisha jumla ya timu saba kutoka katika Kata ya Madimba, Ziwani  na Msimbati wilayani Mtwara kwa lengo la kuendelea kujiweka karibu na jamii.
Afisa usalama wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mihayo Libubu amesema kupitia mashindano hayo vijana watapata fursa ya kupima magonjwa yasiyoambukiza pamoja na Ukimwi hiyari.
“Kama TPDC tumeona ni vyema tukashirikiana na jamii zinazotuzunguka kwa maana ya kwamba tuwe na bonanza la michezo ambalo litatufanya tuzidi kufahamiana nakuwa wamoja zaidi. Mchezo siku zote ni afya unakufanya unakuwa imara lakini sambamba na bonanza hili litakwenda sambamba na kampeni za upimaji kwa hiari, watu waje kwa wingi tuweze kujua afya zetu,”amesema Libubu.
Uzinduzi huo umefanyika kwa kushuhudia mechi iliyohusisha timu za Madimba Kombaini na Ruvula City, ambapo makocha wa timu hizo wakatoa mitazmo yao juu ya mashinddano hayo na lengo lake.
Kocha wa Madimba Kombaini Vintan Kosmeli amesema “Kampeni ya upimaji ni nzuri kwa mimi binafsi sina tatizo kwa sababu sio mara ya kwanza, ila tatizo lio kwa vijana wengi wakiambiwa suala la kupima mioyo yao inadunda, niwashauri watambue tu kwamba kutambua afya zao ni moja ya ushindi katka maisha yao,” amesema.
Naye kocha wa Ruvula City, Omary Hamis amesema timu nyingi za vijijini zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa vifaa kama jenzi, viatu na mipira na kwuaomba wadau kujitokeza kuziwezesha timu za vijijini.
“Naomba wadau na viongozi watsaidie tupate vifaa ndio changamoto kubwa, mfano viatu tunavyotumia havina ubora na haviendani na uchezaji wa mpira,” alisema Hamis.
Mshindi wa michuano hiyo atapatiwa zawadi ya vifaa vya michezo pama na mbuzi mmoja.