THE END

Muktasari:

Dili la Zlatan kwenda Galaxy linatazamiwa kuwa mkataba wa Pauni 1 milioni kwa mwaka na lilitazamiwa kutangazwa kama tangazo katika ukurasa mzima wa gazeti maarufu la Marekani, Los Angeles Times na alitazamiwa kwenda California kwa ajili ya kutambulishwa.

MANCHESTER, ENGLAND

MAMBO hufika mwisho. Zlatan Ibrahimovic na Manchester United wameamua kuchana mkataba uliokuwepo baina yao na staa huyo wa kimataifa wa Sweden jana alitazamiwa kuendelea na maisha mengine kwa kujiunga na klabu ya LA Galaxy.

Dili la Zlatan kwenda Galaxy linatazamiwa kuwa mkataba wa Pauni 1 milioni kwa mwaka na lilitazamiwa kutangazwa kama tangazo katika ukurasa mzima wa gazeti maarufu la Marekani, Los Angeles Times na alitazamiwa kwenda California kwa ajili ya kutambulishwa.

Zlatan mwenye umri wa miaka 36 amesaini mkataba mpaka mwishoni mwa msimu na anaweza kucheza mechi yake ya kwanza kwa wababe hao katika pambano la Ligi Kuu ya Marekani dhidi ya watani wao wa jadi LAFC Machi 31.

United ilithibitisha jana kuwa ilikuwa imeukomesha mkataba wa staa huyo ambaye kwa mara ya kwanza sasa atacheza nje ya Bara la Ulaya baada ya kutamba katika Klabu za Barcelona, Ajax, Paris Saint-Germain, Juventus, Inter Milan na AC Milan.

Zlatan mwenyewe aliandika katika mtandao wake akisema: “Mambo mazuri hufika mwisho na huu ni wakati wa kuendelea na maisha mengine baada ya kuwa na misimu mizuri miwili na Manchester United.

“Asante sana kwa klabu, mashabiki, timu, kocha na wafanyakazi wengine ambao walishirkiana nami katika sehemu hii ya historia yangu…”

Zlatan alikuwa akihusishwa kwa muda mrefu kujiunga na klabu hiyo ambayo iliwahi kuwachukua David Beckham na Steven Gerrard katika nyakati mbalimbali na sasa Zlatan anakwenda kufungua ukurasa mpya klabuni hapo.

Katika msimu wake wa kwanza na Manchester United baada ya kujiunga kama mchezaji huru akitokea PSG, Zlatan alifunga mabao 28 na kuwa mfungaji bora Old Trafford lakini msimu huo ulitibuliwa alipoumia goti vibaya katika pambano la michuano ya Europa Aprili mwaka jana.

United ilitangaza kutomuingiza katika kikosi chake lakini Novemba alipewa mkataba mpya wa mwaka mmoja kwa ajili ya kutoa changamoto kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Romelu Lukaku lakini hakuweza kurudi kuwa fiti tena.

Mechi yake ya mwisho kwa United msimu huu ilikuja Desemba 26, katika pambano dhidi ya Burnley Old Trafford ambapo aliuamia na majeraha hayo yangemuweka nje kwa mwaka 2018. Kocha wake, Jose Mourinho alidokeza mchezaji huyo angeondoka mwishoni mwa msimu lakini United imethibitisha kuondoka kwake mapema zaidi.

“Wote tunadhani huu utakuwa msimu wake wa mwisho kukipiga Manchester United na yatakuwa maamuzi yake binafsi kuendelea kucheza soka au kuacha. Majeraha yale mabaya yaliyokuja katika kipindi ambacho sio mwafaka ndio ambayo yaliharibu misimu mingi mizuri ambayo tungeweza kuwa naye,” alisema Mourinho.

“Kwa sasa sio majeruhi. Anajisikia kuwa na furaha, tayari, na kushawishika kwamba hali yake inaweza kuisaidia timu kwa sasa? Hapana. Lakini ni mtu mkweli na ni mshindi. Anataka kurudi pale tu atakapojisikia ‘Nipo tayari kucheza’,” aliongeza Mourinho.

Ibrahimovic anaweza kukumbana na timu yake ya zamani Manchester United katika mechi za maandalizi ya msimu mpya wakati United itakaposafiri kwenda Marekani kwa maandalizi ya msimu mpya ujao.

Kwa sasa Zlatan anatazamiwa kukipiga sambamba katika klabu yake mpya na beki wa zamani wa Arsenal, Chelsea na timu ya Taifa ya England, Ashley Cole ambaye yupo klabuni hapo sambamba na mchezaji wa zamani wa Tottenham, Giovano dos Santos.