Ndimbo aibukia TFF

Muktasari:

TFF imeanza mpango wa kupanua kitengo cha habari kwa lengo la kuboresha utendaji wake

Dar es Salaam. Afisa habari wa zamani wa Simba, Clifford Ndimbo sasa atakuwa Afisa Habari mpya wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuanzia jana Jumatatu kwa mujibu wa taarifa  kutoka ndani ya shirikisho hilo.
Mmoja ya viongozi wa TFF aliyekataa jina lake kuandikwa ameuambia Mtandao wa Mwanaspoti.com kuwa Ndimbo atakuwa akishirikiana na Alfred Lucas katika kitengo cha habari cha shirikisho hilo.
 “Ndimbo ameanza kazi jana Jumatatu na atashirikiana na Alfred Lucas katika majukumu ya  kitengo cha idara ya habari ambayo moja ya idara muhimu kwa sasa,” kilidai chanzo hicho.
"Unajua kitengo cha habari cha TFF, sasa kimetanuka kwa kiwango kikubwa, kuna Afisa Habari na masuala mengine kama mitandaoni na kadhalika hivyo hawa mabwana inabidi wasaidiane," alisema mtoa taarifa wa kuaminika ndani ya TFF.
Alipoulizwa Ndimbo kuhusu taarifa hiyo alishindwa kukataa wala kukubali suala hilo akitaka watafutwe TFF wenyewe waseme.
“Linaweza kuwa kweli au lisiwe kweli ila wenye mamlaka ya kuthibitisha hilo ni viongozi wa TFF,” alisema Ndimbo.
Mtu wa karibu wa Ndimbo alithibitisha kuwa jambo hilo ni la kweli na ameshaanza kazi TFF chini ya Rais Walles Karia.
“Kweli ameanza kazi na kwa taarifa za awali atakuwa anafanya kazi kwa kusaidiana na Alfred, ambaye alikuwepo katika nafasi hiyo na kama mabadiliko yatafanyika hapo baadae,” alisema rafiki wa karibu wa Ndimbo.
Alipotafutwa Afisa Habari wa TFF, Lucas kuthibitisha taarifa hiyo simu yake haikupatikani.