TFF yaingia matatani Arachuga

Muktasari:

  • Tanzanite FC wametoa malalamiko hayo baada ya kuingia kambini mapema Mei mara baada ya TFF kutangaza kuanza kwa michuano ya Ligi Ndogo ya Wanawake iliyotakiwa kuanza Julai 16 jijini Tanga.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) imeingia lawamani baada ya timu ya Soka ya Wanawake, Tanzanite FC kulilalamikia kwa kitendo chao cha kupangua ratiba ya Ligi ya Wanawake na kuwabebesha mzigo usio wa lazima.

Tanzanite FC wametoa malalamiko hayo baada ya kuingia kambini mapema Mei mara baada ya TFF kutangaza kuanza kwa michuano ya Ligi Ndogo ya Wanawake iliyotakiwa kuanza Julai 16 jijini Tanga.

TFF walitangaza kuahirisha kwa mara nyingine na kwamba michuano hiyo ingeanza kutimua vumbi keshokutwa Jumamosi, lakini wameahirisha kwa mara ya nne kwamba itaanza Septemba 8 lakini sasa yametangazwa kufanyika mwezi ujao kwa tarehe itakayotangazwa hapo baadaye.

Meneja wa Taasisi ya Tanzanite 2014, George Mtembei inayomiliki timu hiyo pekee ya wanawake kutoka Arusha iliyopo Ligi Kuu ya Wanawake alisema kuahirishwa huko kunawapa wakati mgumu na kulazimika kuanza kuomba msaada kwa wadau ili kuendelea kumudu gharama za maandalizi.

“Kuweka timu kambini muda wote wakila na kulala na kufanya mazoezi bila kujua tarehe rasmi ya mashindano ni gharama sana.

“Hali hii inatupa wakati mgumu, TFF wanapaswa kuliangalia hili kwa umakini mkubwa,” alisema Mtembei.

Alisema kama klabu walishapanga bajeti ya mashindano na kuanzia maandalizi lakini bajeti zote zimevuruguka kutokana na hali iliyojitokeza kutokana na mipango ya TFF ambayo kila mara ratiba ya kuanza inasogezwa mbele bila msingi.