TFF na timu za Ligi Kuu bara msife moyo

Ni habari ambazo haziwezi kuwa nzuri kusikika kwa wapenzi wa mpira wa miguu pamoja na timu shiriki katika ligi kuu ya Tanzania bara kwamba ligi yetu bado haijapata mdhamini mkuu mpaka sasa. Hili linakuja huku zikiwa zimebaki siku kadhaa kabla ya kipenga cha kwanza katika msimu wa 2018/19 kupulizwa baada ya waliokuwa wadhamini wakuu, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom kumaliza mkataba wake wa miaka mitatu wa kuidhamini ligi yetu.

Jambo hili linaonekana kuugusa umma wa wanamichezo pamoja timu kwani hakuna mtu asiyetambua gharama za kuendesha timu katika kushiriki ligi kuu, hakuna asiyefahamu nafasi iliyokuwa nayo kampuni ya Vodacom katika kufanikisha ligi hii. Hata hivyo kama Waswahili wasemavyo, hakuna marefu yasiyo na ncha na ndivyo ambavyo mdhamini wa ligi kuu kwa miaka kadhaa iliyopita alivyofika kikomo lakini ligi ndiyo kwanza inaanza.

Hata hivyo katika wakati huu ambao pengine tutashuhudia mengi kwa timu zetu ukizingatia kwamba msimu wa 2018/19 utakuwa na timu 20, ni dhahiri kuwa timu pamoja na wapenzi wa soka watapitia kipindi fulani hivi ambacho kitakuwa kichungu kama shubiri. Nasema hivi kwa sababu tunafahamau hali halisi ya timu zetu. Kwa sasa timu nyingi ukiacha timu ambazo kwa namna moja ama nyingine zina watu na makampuni yanayoweza kuwashika mkono kama Simba, Azam na Yanga ambayo hata hivyo nayo bado haijasimama, timu nyingine zitapata tabu kwa kiasi kikubwa.

Viongozi kadhaa wa timu shiriki katika ligi hii ikiwemo Singida United, African Lyon pamoja na Alliance wamekiri wazi kuwa itawawia vigumu kumudu gharama za undeshaji wa timu katika mashindano haya kwani mdhamini mkuu alikuwa msaada kwa kiasi kikubwa. Pamoja na hayo wapo wachambuzi na wachezaji wa zamani wameliona hili, kwamba wakati huu unaweza kushusha ushindani kwa baadhi ya timu kwani itapunguza ari na hamasa kwa wachezaji wawapo uwanjani. Mmiliki wa African Lyon, Bw. Rahim Kagenzi “Zamunda” alinukuliwa hivi karibuni akieleza wazi kwamba kuna uwezekano wa baadhi ya malengo watashindwa kuyafikia kwa sababu ya kukosekana kwa mdhamini mkuu.

Mwenyekiti wea Shirikisho la soka nchini, Walace Karia pamoja na bodi ya ligi (TPLB) naO wanaonekana kuguswa moja kwa moja na hili jambo ambalo wanasisitiza timu zisikate tamaa kama ambavyo TFF hawakati tamaa kwa wanendelea kutafuta udhamini.

Ndiyo,ni kweli kabisa kuwa hatupaswi kukata tamaa, nyakati huja na kupita, tumeshuhudia timu mbalimbali zikipitia nyakati kama hizi ikiwemo Yanga lakini bado Yanga ipo haijafa na pengine bado ina nguvui ileile. Wakati TFF ikiendelea kutafuta wadhamini timu ziendelee kujiandaa kwani lolote linaweza kutokea, hatupaswi kukata tamaa na kuona kama hatuwezi kuendelea.

NINI KIFANYIKE?

Huu ni wakati wa timu ambazo zinahisi zitasumbuka au kushindwa kumudu gharama kushikamana na kujiandaa kisaikolojia ili ziweze kukabiliana na athari ambazo zitatokea ikiwa ligi itaanza bila mdhamini. Kwa kufanya hivi tutajifunza kukabiliana na hali halisi kutoka ndani kabla ya kutokeza kwa nje.

TFF isikate tamaa, iongeze juhudi kutafuta makampuni zaidi ikiwezekana hata mashirika ya kimataifa hata kama hawatapata kampuni au shirika litakalokuwa mdhamini mkuu lakini yakawa mengi na hela zitakazopatikana zikakusanywa kidogokidogo walau zitakuwa msaada.

Viongozi wa timu mbalimbali wasianze kukwepa majukumu kwa kujiuzulu au kutupia mipira bali wakubali kwamba timu ni zao, waende kwa wananchi na mashabiki waeleze ukweli ikiwezekana wafanye changizo ambazo zinaweza kuwa msaada kwa timu. Hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wa klabu hasa Yanga wakijiuzulu kwa sababu ya kipindi kigumu inachopitia timu bila kufahamu kwamba kwa kufanya hivo kunaongeza tatizo na kushusha morali ya wachezaji.

Uvumilivu wa mashabiki ni jambo lingine la msingi sana. Mashabiki wengi wa soka huwa wanapenda timu ifanye vyema, ishinde kila mchezo hata kama wanafahamu mpira wa miguu una matokeo matatu. Inapotokea timu inapitia wakati mgumu basi mashabiki hukosa uvumilivu na kuanza kuongea lolote lile linalokuja kinywani, kwa kweli tutazidi kuharibu. Katika kipindi hiki ambacho shirikisho linatafuta wadhamini, mashabiki tuzibebe timu zetu, tuvumilie, tuwavumilie viongozi kwani wao pia wanatiwa nguvu na msukumo wetu mashabiki.

Jambo la mwisho, kupitia hili tutafakari namna ya kuziendesha timu zetu katika mfumo ambao timu zitaweza kujiendesha hata kama changamoto kama hii itajitokeza. Ufike wakati tuone kuna haja ya timu kuwa na vitega uchumi ambavyo vinaweza kuwa sehemu ya kukusanyia mapato. Hivi sasa zipo timu ambazo kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na watu au makampuni binafsi kama Azam na Simba ambayo hivi karibuni imechukuliwa na mwekezaji Mohammed Dewji ingawa si kwa 100% lakini zinaweza kuhimili mtikisiko huu, ni vyema timu nyingine zikafuata mfumo huu.

Tuwe wavumilivu na tujiandae kukubaliana na hali yoyote ili tuweze kukabiliana na hali hii ikiwa itabaki kuwa hivi ingawa nina imani na shirikisho letu la mpira wa miguu (TFF) chini ya mwenyekiti wake Walace Karia. Bado tunaweza kufanikiwa kuziendesha timu na ligi, tusijihisi wakiwa, tusione kama tumeshindwa. Kwa wale viongozi ambao wanaona kama morali ya timu zao zitashuka pamoja na kutokufikia malengo wasikubali kuvunjwa moyo wa kupambana.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

0672395558.