Sugu aikumbuka siku aliyovuliwa nguo zote gerezani-2

Muktasari:

  • Anasema siku iliyokuwa ngumu kwake kuliko zote akiwa gerezani, ni alipovuliwa nguo zote hadharani na askari kabla ya kumpekua wakimshutumu kuwa alikuwa ana simu.

Mbeya. Maisha ya gerezani huwa si mazuri, hakuna anayependa kwenda jela. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amekaa gerezani kwa siku 73, lakini mwanamuziki huyo wa hip hop, anasema katika siku hizo, kuna siku moja tu ambayo hawezi kuisahau.

Anasema siku iliyokuwa ngumu kwake kuliko zote akiwa gerezani, ni alipovuliwa nguo zote hadharani na askari kabla ya kumpekua wakimshutumu kuwa alikuwa ana simu.

Sugu na katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walikuhumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 baada ya kukutwa na hatia ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Waliachiwa huru Mei 10 kwa msamaha wa Rais alioutoa siku ya sherehe za Muungano Aprili 26, jijini Dodoma.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Sugu anasema yeye na mwenzake Masonga hawataisahau siku hiyo kwa madai walidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo zote hadharani na askari.

‘Siku iliyokuwa ngumu kwangu na niliyokasirika sana ni siku ambayo askari walitulazimisha kuvua nguo ili kutukagua. Siku hiyo tulitoka mahakamani na tulipofika gerezani tukaambiwa kuna agizo toka juu kwamba tukaguliwe mpaka tuvuliwe nguo.

“Sasa haijalishi kuvua nguo kwa sababu pale ni wanaume watupu hata vyoo vyenyewe havina milango viko wazi…. Lakini sasa unapomvua nguo mtu mbele ya hadhara ya zaidi ya wafungwa 1000 wamezunguka wanakuangalia huko sio ‘ku-search’ (kupekuliwa) bali ni dhamira ya kumdhalilisha mtu kumfanya ajione si chochote na si lolote……. Kwa hiyo kilinikera sana kitendo kile,” anasema Sugu.

Anasema ndani ya gereza hilo kuna watoto wadogo wa umri wa miaka 15 hadi 16 wamefungwa na wamechanganywa kwenye ‘selo’ moja na watu wazima hivyo kwa umri wake na watu wengine wenye umri mkubwa anadhani si sawa kuvua nguo mbele ya watoto kwani ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Kama unataka kupekuwa watu basi tengeneza chemba (chumba maalumu) kwa sababu mtu hata akiwa ni mfungwa haimuondolei ubinadamu na haki zake za msingi. Metal detectors (vifaa vya ukaguzi) wanavyo sasa ya nini uanze kumvua mtu nguo na kuanza kumpekuapekua? Unataka kuangalia nini!!!.... Unajua kitendo kile hadi nikajiuliza hawa askari vipi wenye …. kupekua pekua wanaume wenzao? Kwa hiyo siku hiyo kwa kweli nilijisikia vibaya kidogo,” anasema.

Anasema katika maisha yake akiwa gerezani hakuwahi kufikiria kushika simu na hakuhitaji kufanya hivyo kwani muda mwingi marafiki, wananchi wa kawaida, viongozi mbalimbali walikuwa wakimiminika gerezani hapo kumjulia hali hivyo kila kitu kilichokuwa kikiendelea nje alikuwa akipewa.

“Sikuwahi fikiria kushika simu nikiwa gerezani. Na sikuhitaji kabisa kwa sababu hapa (Mbeya) ni nyumbani kwa hiyo ndugu, familia, marafiki, wananchi wa kawaida, wabunge wenzangu na viongozi mbalimbali walikuwa wanakuja kila wakati kunijulia hali, hivyo kila kitu nilikuwa nakipata na nilipohitaji kutoa agizo la kitu fulani kitekelezwe nilifanya hivyo kwa kuzungumza nao gerezani,” anasema.

Tofauti yake na wafungwa wenzake

Akizungumzia hali ilivyokuwa kwa mara ya kwanza alivyoingia gerezani, Sugu anasema ilitokea sintofahamu kwa wafungwa wenzake kwani walishtuka kumuona akiingia ndani kama mfungwa jambo ambalo lilimlazimu ajishushe ili kuwatuliza.

“Kwanza wafungwa mle ndani walishtuka kuniona… na isingekuwa kujishusha ilitaka kutokea mtiti (vurugu) ndani ya gereza, lakini nilikaa nao nikawaeleza kwanini nipo mle ndani, nikawaambia msiogope na ndipo nchi ilipofika kwa sasa, lakini pia askari nao wakaja wakawatuliza basi wakaelewa na maisha yakaendelea kama kawaida,” anasema rapa huyo.

Anasema hali hiyo ilimfanya ajione mtu wa tofauti na anayekubalika na watu wote hata waliopo ndani ya gerezani kwa sababu kitendo cha kuingia gerezani, kiliwafanya wafungwa wengine kutoridhika.

Sugu anasema tofauti nyingine aliyoiona akiwa gerezani ni wafungwa wenzake pamoja na askari magereza kuendelea kumtambua na kumheshimu kama mbunge wao na siku zote walikuwa wakimuita ‘mheshimiwa’.

“Yaani mle kama vile kulikuwa na jimbo ndani ya gereza, muda wote niliokaa gerezani na wafungwa niliitwa mheshimiwa na si jina jingine.”

Anasema asilimia 97 ya askari wa magereza aliishi nao vizuri na walimpa ushirikiano mkubwa na wao walitimiza wajibu wao kwa weledi huku akimweleza shida zao na kumtaka asione kama wanamnyanyasa kwa utashi wao.

“Ukiachana na askari ‘wadwanzi’, wachache kama wale waliokuja na kutulazimisha tuvue nguo, asilimia 97 niliishi nao vizuri sana na niliwaambia wasihofu kwani walionileta ndani sio wao bali wapo nje hivyo humu ndani tuendelee na maisha kama kawaida. Hivyo waliendelea kunitambua mimi kama mbunge wao, na hizo ndio tofauti niliziona mle ndani.”

Anasema hakuwa na shida na askari magereza kuona wanamheshimu kwani anajua ni wapiga kura wake na kwamba hata katika chaguzi mbili zilizopita mitaa ya magereza ambako askari magereza na askari wa kawaida wanaishi huwa anaongoza kwa kura.

Ratiba yake ilikuwaje?

Akizungumzia ratiba yake na wafungwa wengine, Sugu anasema kila siku saa 1:00 asubuhi selo hufunguliwa na wafungwa wote hutoka kwenda kufanya shughuli wanazokuwa wamepangiwa hadi saa 9:00 alasiri hupigwa miluzi ya kuashiria muda wa kulala umefika.

“Muda wa kula chakula ni kati ya saa5:00 asubuhi hadi saa 8:30 mchana, labda ikitokea changamoto ya chakula kuchelewa kuiva kwa sababu ya kuni zilizolowa na mvua inaweza kufika hadi saa 11:00 jioni bado hamjafungiwa.”

Anasema katika kipindi chote alichokaa gerezani, aliona muda mwingi unaotumika kwa wafungwa ni wa kukaa ndani kuliko kuwa nje huku akisisitiza kwamba hakuna siku aliliona giza kwani alikuwa akiingia wakati wa mwanga na anatoka nje kukiwa na mwanga.

Siku ya kuzaliwa gerezani

Sugu alisherehekea siku yake ya kuzaliwa Mei Mosi, ‘Siku ya Wafanyakazi duniani’ akiwa gerezani akiendelea kutumikia kifungo cha miezi mitano.

Katika kusherekea siku hiyo, Sugu anasema alisherekea ‘kiaina’ na wafungwa wenzake waliokuwa selo moja na wengine wa selo jirani .

Anasema aliiona siku hiyo muhimu zaidi kwa jinsi familia yake ikiongozwa na mke wake Happines Msonga walivyokwenda kula chakula cha pamoja na watoto yatima katika kituo cha Nuru kilichopo Uyole ya Kati jijini hapa.

“Siku yangu ya kuzaliwa niliiona imekwenda vizuri zaidi kwa kuona familia yangu na uongozi wa Hoteli ya Desderia ulivyokwenda kufanya kile walichokifanya kwa watoto yatima kwa kula nao chakula cha pamoja na kuwapelekea baadhi ya misaada mingine. Kwa kweli ile ilinifanya nijisikia amani na ilinipa faraja sana kwa siku ile kuliko kitu chochote.”

Anasema kitu kingine kilichomfanya ajisikie tofauti ni kitendo cha kupelekewa zawadi ya keki gerezani ikiwa imepambwa kwa kuchorwa pingu na picha yake ikionekana kupitia nondo za keki hiyo kwani anasema ni kitu ambacho hakukitarajia.

“Ile keki sikuijua wala sikuitarajia hivyo nilifanyiwa ‘surprise’ ya kufa mtu aisee, lakini siku zote ipo hivyo ni kama vile mke wangu tumeshazoeana, ananijulia sana na mara nyingi huwa anakuwa na ‘surprise surprise’ zake. Hivyo ni mtu anayenijua hivyo siku ile alifanya kitu sahihi kabisa na nikala ile keki pamoja na wafungwa, wengine ni wafungwa masikini kabisa na pia kuna askari walishiriki kula ile keki kwa hiyo ‘birthday’ ilikuwa sawa sawa na ilitimia.”

Anasema suala la uongozi wa hoteli yake na familia yake kwenda kula chakula na watoto yatima ilikuwa ni agizo lake, lakini wao walijiongeza zaidi kwa kupeleka zawadi kwa watoto hao, jambo ambalo amedai lilimpa faraja kubwa akiwa gerezani.

Itaendelea kesho