Straika mpya kuwadhibiti mabeki visiki Ligi Kuu

Muktasari:

Ligi kuu imekuwa na mabeki wanaosifika kwa ukabaji  na ubabe akiwemo mlinzi wa Yanga, Kelvin Yondani ambaye msimu uliopita alikuwa msaada mkubwa kwa klabu yake.

IKO hivi Straika mpya wa Biashara United, Austine Amos ambaye ni raia wa Ivory Coast amesema ametonywa kuhusu  ugumu na ubabe wa Mabeki wa Ligi Kuu lakini hilo halimumizi kichwa kwani malengo yake ni kufunga kila mechi watakayocheza kwani hiyo ndio kazi yake iliyomleta Bongo.
Ligi kuu imekuwa na mabeki wanaosifika kwa ukabaji  na ubabe akiwemo mlinzi wa Yanga, Kelvin Yondani ambaye msimu uliopita alikuwa msaada mkubwa kwa klabu yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Amos alisema anajua ugumu wa mabeki wa Ligi kuu kwani amepewa taarifa zao lakini yeye amekuja kwa jambo moja la kuhakikisha anatupia mabao kila mechi.
Alisema kwake ana wasiwasi na mabeki hao kwani amejipanga vilivyo kuhakikisha anaipa mafanikio timu hiyo kwa kufunga mabao yatakayomfanya aibuke mfungaji Bora wa Ligi.
“Najua Ligi ya Tanzania ina mabeki wagumu sana hilo nilishaambiwa nalijua lakini mimi kazi yangu iliyonileta  ni kufunga mabao hakuna kingine tutapambana uwanjani”alisema Amos.
Kwa upande wake Kipa Balora Nourdine aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuwapa sapoti ambapo amesema hilo litawapa wao nguvu katika safari ya kuipa mafanikio timu hiyo.
“Tumekuja kuipa mafanikio Biashara United lakini hili litafanikiwa kama sote tukiwa kitu kimoja kuanzia wachezaji hadi mashabiki”alisema Nourdine.
Biashara United kwa sasa wako katika maandalizi ya kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ambapo timu hiyo ya Mkoa Mara itashiriki Michuano hiyo kwa mara ya kwanza.