Straika Yanga anacheeeka kwa zile bao

Muktasari:

Martin ni kama alitoa gundu la kutofunga baada ya kutupiamabao hayo ambayo ndio anayoyamiliki mpaka sasa katika mechi 10 alizocheza msimu huu.

MABAO mawili aliyofunga Emmanuel Martin wakati Yanga ikishinda 5-0 dhidi Mbeya City juzi Jumapili, yamempa sauti mchezaji huyo aliyesema yamemtoa kifungoni na kumpa amani ya moyo.

Martin ni kama alitoa gundu la kutofunga baada ya kutupiamabao hayo ambayo ndio anayoyamiliki mpaka sasa katika mechi 10 alizocheza msimu huu.

Hakusita kueleza ukweli namna alivyokuwa anajisikia vibaya kutofunga bao hata moja katika mechi tisa, kwani alijiona mchango wake hauonekani.

“Asikwambie mtu, Yanga ni klabu inayotetea ubingwa, kama straika nilikuwa naumia sana nikitoka kapa bila kufunga, hilo lilikuwa linavuruga hadi akili yangu,” alisema.

“Mbeya City imenifungulia njia ya kujiamini zaidi, kabla ya mzunguko wa pili naweza nikawa na mabadiliko ya hali ya juu katika nafasi yangu ya ufungaji.”

Kwa upande wa winga wa zamani wa timu hiyo, Ally Yusuph ‘Tigana’, alisema kuwafunga City mabao 5-0 ni kama kumepunguza nguvu ya Simba.

“Yanga wakishinda kwa staili hiyo katika mechi mbili au tatu zijazo basi Simba, watakuwa hawana jipya, la sivyo wapambane sana kuhakikisha wanaongeza umakini kwenye umaliziaji,” alisema mchezaji huyo aliyekuwa matata enzi zake uwanjani.