Straika Mwanza autaka ufungaji bora Copa Umisseta

Muktasari:

Paul  ameshafunga mabao sita na kuiongoza Mwanza kuongoza kundi lao katika kituo cha Nsumba kwa pointi 12 baada ya mechi nne walizocheza.

Mwanza. Mshambuliaji chipukizi wa timu ya soka ya Mkoa wa Mwanza, Kelvin Paul ameendeleza makali yake ya kuzifumania nyavu katika michuano ya Umoja wa michezo kwa Shule za Sekondari nchini (Copa Umisseta) inayoendelea jijini hapa.

 

Paul  ameshafunga mabao sita na kuiongoza Mwanza kuongoza kundi lao katika kituo cha Nsumba kwa pointi 12 baada ya mechi nne walizocheza.

 

Nyota huyo ameonekana kuwavutia hata timu zingine, kutokana na ufungaji wake  huku akitoa pasi za mwisho za  mabao mengine waliyofunga wenzake.

 

Juzi wakicheza dhidi ya Arusha, alifunga bao moja wakati Mwanza ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kuendeleza rekodi ya kushinda mechi zote.

 

Akizungumzia rekodi hiyo, Paul alisema kiu yake ni kuibuka mfungaji bora katika michezo hiyo inayoshirikisha wanafunzi zaidi ya 3,000.

 

"Ushindani upo, lakini kikubwa nafuata maelekekezo ya kocha na kiu yangu ni kuwa mfungaji bora wa michezo hii na kuendeleza kipaji changu"alisema Paul.

 

Naye Kocha wa Mwanza, Mathias Wandiba alisema mshambuliaji huyo anaonyesha uwezo wake na kwamba amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu.

 

"Hata kama hatushindani hapa, lakini kubwa ni kuwandaa vijana kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, kwahiyo nitapambana kuhakikisha nafanikisha hilo"alisema Wandiba.

 

Matokeo mengine ya Soka kwa Wasichana, Mwanza ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Tabora, Netiboli Mwanza ikailaza Katavi mabao 44-19 na kwenye Kikapu,Pwani ikaichapa Rukwa mabao 101-14.