Stand United, Yanga ni vita ya kisasi

Muktasari:

  • Yanga itashuka kwenye Uwanja Kambarage ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa hapo msimu uliopita

Stand United itakuwa na kazi moja tu kurudi rekodi nzuri dhidi ya Yanga Jumapili hii kwenye Uwanja wa  Kambarage mjini Shinyanga.

Msimu uliopita Yanga kwa mara ya kwanza ilikubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja huo shukrani kwa bao la Pastory Atanas ambaye kwa sasa yupo Singida United.

Hivyo mchezo wa Jumapili utakuwa mgumu kwa timu zote mbili kwani Yanga wanataka kulipiza kisasi cha msimu uliopita na kujiweka vizuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Stand United wanataka kupata ushindi ili kujinasua mkiani kwani mpaka saa wana pointi nne huku wakiwa katika nafasi ya 15.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Agustino Malindi alisema watawashangaza Yanga kama walivyofanya msimu uliopita kwa kuwa kikosi chao kimeimarika siyo kile kilichoanza Ligi.

Alisema walisajili wachezaji damu changa ambao mwanzoni walikuja hawajazoea ligi, lakini sasa wameimarika hivyo lazima mchezo huo wanyakuwa pointi tatu.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema wao wako tayari kwa mechi zote za Ligi kuu katika mzunguko wa kwanza kwani mipango yao ni kutaka kutetea ubingwa.

“Tuko tayari kutetea ubingwa wetu hivyo tumejipanga kwa mechi zote kuweza kupata ushindi hatuangalii mchezo mmoja mmoja,”alisema Nsajigwa.