Sserunkuma wa Simba apata ulaji mpya Morocco

Muktasari:

Mshambuliaji huyo ameachana na FC Bandari ya Kenya na kujiunga na Tangier inayopatikana katika pwani ya Morocco.

Kampala, Uganda. Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Daniel Sserunkuma amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na klabu ya Ittihad Riadi Tanger inayoshiriki ligi daraja la kwanza (Botola ligi) Morocco.

Mshambuliaji huyo ameachana na FC Bandari ya Kenya na kujiunga na Tangier inayopatikana katika pwani ya Morocco.

Sserunkuma alituma katika ukurusa wake wa twitter kuthibisha uhamisho huo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo;

"Nairobi-London-Spain-Morocco. Kwa hiyo Morocco si ndiyo!!! Kuanzia sasa mimi ni mchezaji wa Ittihad Riadi Tanger!!!

"Sifa kwa Mungu. Napenda kuwashukuru familia yangu, wakala na mashabiki wote wanaoniunga mkono.

Sserunkuma pia alitoa shukrani kwa klabu yake ya zamani, "Asanteni Bandari FC kwa upendo wote na kuuniunga mkono wakati wote, niwatakie mafanikio mema!

Mshambuliaji huyo amecheza kwa msimu umoja Bandari, iliyomsajili akitokea klabu ya nchini Armenia, Ulisses Football Club.

Nyumbani kwao Uganda amewahi kucheza Express na Victors. Wakati Kenya amezichezea Nairobi City Stars, Gor Mahia na mwisho Bandari.

Katika msimu wa 2014 – 2015, Sserunkuma alichezea Simba ya Tanzania, lakini alishindwa kutamba.