TIA wafalme wa soka Mbeya

Muktasari:

  • Katika michuano hiyo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa timu  bingwa washiriki wengine walipewa vyeti  vya ushiriki wa michuano hiyo mwaka 2017/2018.

Timu ya soka ya Chuo cha Uhasibu Tanzania  (TIA) tawi la Mbeya wameibuka mabingwa wa michuano ya vyuo vyote vya Mkoa wa Mbeya kwa mwaka wa 2017/2018 na kujinyakulia kitita cha Sh300,000 na kombe  baada ya kuinyuka klabu ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) tawi la Mbeya kwa bao 1-0.

Bao pekee ya ushindi kwa TIA lililofungwa na mshambuliaji wake, Felisian Tonelo dakika ya 19 ambapo mchezo huo ulichezewa Uwanja wa Chuo Kikuu Teofilo Kisanjia (Teku)-Mbeya na katika michuano hiyo ambayo ilidhaminiwa na kituo cha radio cha Dream FM ilishirikisha vyuo nane vya mkoani hapa.

Mpambano mwingine katika fainali hizo, ulikuwa ni upande wa Netiboli ambao uliwakutanisha timu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya, (Must) na SAUT ambapo MUST waliibuka na ushindi wa mabao 17-9 na kufanikiwa kunyakua kombe la Dream Intercollege lililoandaliwa na Radio Dream ya jijini hapa.

Waziri wa Michezo kutoka Saut, Mwegane Yeya alisema walijipanga kuchukua ubingwa wa michuano hiyo lakini dakika 90 ziliamua mshindi na bahati ilikuwa kwa majirani zao TIA.