Siri ya fainali Kombe la FA kuchezwa Arusha

Muktasari:

Fainali hiyo inayotarajiwa kuchezwa Juni 2 jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheik Amri Abeid

Arusha. Mjumbe wa kamati ya mfuko wa maendeleo ya soka TFF, Athumani Kihamia amefichua siri ya shirikisho hilo kuipa nafasi mkoa wa Arusha kuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam mwaka huu.

Kihamia alisema lengo ni kuinyanyua Arusha kutoka katika usingizi mzito waliolala kwa muda mrefu kisoka, hivyo wanaamini kuyahamishia mashindano makubwa katika mkoa huu utaleta hamasa na chachu ya wadau kuamka.

Fainali hiyo inayotarajiwa kuchezwa Juni 2 jijini Arusha kwenye Uwanja wa Sheik Amri Abeid, Kihamia alisema endapo Arusha itarudi katika hadhi yake ya awali mbali na kuleta burudani kwa wadau wa michezo, lakini itaongeza mapato ya TFF taifa na mkoa.

“Unajua kwa sasa tunaangalia namna ya kuendeleza mchezo wa soka katika mikoa yote, na mimi nikiwa mjumbe wa kamati ya mfuko wa maendeleo ya mpira wa miguu naanza na Arusha maana ndio makazi yangu kuhakikisha tunakuwa na uwakilishi ligi kuu maana ndio maendeleo yenyewe ya soka hayo.”

Kihamia ambae pia ni mkurugenzi wa jiji la Arusha amesema kuwa maendeleo ya soka ni wingi wa timu za mikoa kushiriki mshindano makubwa ya kitaifa na kimataifa hivyo wameona mkoa huu una nafasi kubwa ya kupaa kisoka kutokana na historia yake ya nyuma

“Arusha ilikuwa na timu zaidi ya tatu ligi kuu miaka ya nyuma sijui kwa sasa wamekumbwa na nini hivyo naamini nitaacha historia kwa kurudisha hadhi ya soka hapa, ndio maana nimepambana kuhakikisha fainali inachezewa hapa na baadae tutafanya maombi mengine hata ligi ya vijana wa ligi kuu ifanyikie hapa.”