Siri ya Yanga kujificha Pemba

Muktasari:

Yanga iliwasili kisiwani Pemba Jumatatu ikiwa na wachezaji 25 pamoja na viongozi wanane kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mashindano ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Zanzibar. Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh amefichua siri ya klabu hiyo kupenda kuweka kambi kisiwani Pemba akisema mara zote wanapotoka visiwani huko wao ni ushindi tu.

Yanga iliwasili kisiwani Pemba Jumatatu ikiwa na wachezaji 25 pamoja na viongozi wanane kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mashindano ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Akizungumzia kambi hiyo Meneja Saleh alisema hiyo ni sababu moja kwao kupenda  kuweka kambi huko hasa kutokana na timu kuwa na hamu ya kushinda kila mchezo na si jambo lingine.

Saleh aliyasema hayo kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba wakati kikosi chake hicho kikiwa kwenye kambi ya wiki moja kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba pamoja na Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Alisema kuwa kikosi chake hadi wakati huu kinaendelea vizuri kimazoezi, isipokuwa wachezaji watatu akiwemo Kelvin Yondani,Youthe Rostand pamoja na Juma Mahadhi ni majeraha lakini hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema jitihada zinafanyika ili kuona wachezaji wote hao wanarudi katika hali zao za kiafya na kuendelea mazoezi na wenzao.