Kocha Ndayiragije aziweka njia Singida, Mbao

Muktasari:

Mkurugenzi wa Singida United, Clement Sanga alisema taarifa zinazosambaa kuwa Ndayiragije anajiunga na klabu hiyo si za kweli kwani hawajafanya mazungumzo naye.

Mwanza. Uongozi wa Singida United umesema hauna mpango wa kumsajili kocha wa Mbao FC, Ettiene Ndayiragije licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa kocha wao Hans Van Pluijm anatakiwa na Azam.

Mkurugenzi wa Singida United, Clement Sanga alisema taarifa zinazosambaa kuwa Ndayiragije anajiunga na klabu hiyo si za kweli kwani hawajafanya mazungumzo naye.

“Hizo taarifa tunazisikia tu kwa watu, lakini nikuhakikishie bado hatujazungumza naye, hata Kocha wetu Pluijm(Hans) naye anahusishwa kwenda Azam, lakini sisi hatujapata uthibitisho,” alisema Sanga.

Sanga alieleza kuwa iwapo itabainika kuwa Mholanzi huyo anatimkia Azam, basi watamtafuta kocha mwingine mwenye uwezo kama wake ili kuanza kazi mara moja.

Mwenyekiti wa Mbao FC, Solly Njashi alisema iwapo Ndayiragije ataamua kutimkia Singida United wao hawamzuii, lakini kikubwa wanahitaji awe muwazi.

Alisema Mrundi huyo bado ana mkataba na klabu hiyo, hivyo kama amepata majukumu mengine atoe taarifa ili aondoke kwa heshima kwani hawana ugomvi naye.

“Tunachotaka awe muwazi, bado ana mkataba na sisi, asifikirie kwamba tuna ugomvi naye, hatuwezi kuzuia riziki yake ila atoe taarifa ili taratibu zingine zifuate,” alisema Njashi.

Juhudi za kumpata Ndayiragije zilishindikana kutokana na simu zake kutopatikana hewani, kwani kocha huyo hajaonekana tangu kumalizika kwa mchezo wao na Lipuli uliomalizika kwa suluhu.