Singida United yawakana Dida, Barthez wa Yanga

Wednesday July 12 2017

 

By Matereka Jalilu, Mwananchi; mjalilu@mwananchi.co.tz

Dodoma. Klabu ya Singida United, imesema haina mpango wa kuwasajili wachezaji watatu kutoka Yanga kama inavyodaiwa.

Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu uliopita inahusishwa na kutaka kuwasajili makipa wawili wa Yanga, Deogratius Munishi 'Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ pamoja na beki Oscar Joshua.

Katibu mkuu wa Singida United, Abuurahman Sima amekana taarifa hizo kwa kusema timu hiyo haina mpango na wachezaji hao. 

“Hizo ni tetesi tu ambazo ni wakati wake ila kwenye uongozi wetu bado hakuna taarifa za timu yetu kumtaka huyo beki {Joshua} wala kipa yeyote kutoka Yanga kwa wakati huu,” alisema Sima.

Wakati Singida United wakisema hayo Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa Yanga, Hussein Nyika amewaahidi mashabiki wa timu hiyo kujiandaa na usajili ‘Babkubwa’ wikiendi hii.

Nyika ametoa ahadi hiyo kwa mashabiki na wapenzi wa Yanga kwamba kamati yake imekamilisha usajili mzito wa kimataifa utakaotikisa nchi mithili ya bomu la nyuklia.

“Usajili wetu tunaoufanya tunalenga zaidi wachezaji wenye uwezo wa kushindana kimataifa na hilo tutalithibitisha wikiendi hii,”alisema Nyika