Simbu awapasua vichwa wapenzi wa riadha

Muktasari:

Unaambiwa hadi amalize mafunzo yake jeshini ni kati ya mwishoni mwa Mei na mwanzoni mwa Juni mbio za London zitakuwa zimeshafanyika kitambo tu kwani zinafanyika Aprili 24.

Dar es Salaam. Kama ulitegemea kumuona Alphonce Simbu kwenye mbio za London Marathoni msimu huu basi pole yako, labda msubiri kwenye zile za 2019 kwani nafasi ya kurejea kwenye riadha ni hadi Juni.

Unaambiwa hadi amalize mafunzo yake jeshini ni kati ya mwishoni mwa Mei na mwanzoni mwa Juni mbio za London zitakuwa zimeshafanyika kitambo tu kwani zinafanyika Aprili 24.

Kocha wa Simbu, Francis John alisema hajui kama Simbu atashiriki mbio hizo, lakini anasikilizia mpango wa jeshi kwa kuwa Simbu yuko kwenye mafunzo.

Simbu hataweza kushiriki mbio za London Marathoni na kama haitoshi, RT na kocha wake waondoe kabisa wazo la kumtumia kwenye mbio hadi Juni.

Akizungumzia mpango huo, nyota wa zamani wa riadha ambaye ni sajenti wa JWTZ, Samson Ramadhani ambaye cheo alichokipata kutokana na kasi ya kufukuza upepo alisema kwa mafunzo ambayo Simbu anapatiwa atakapomaliza ili awe fiti atatakiwa kujifua miezi miwili.