Simba yazindua jezi mpya

Dar es Salaam. Simba imezindua jezi zao mpya watakazotumia msimu huu zikiwa ni tofauti na zile za  msimu uliopita.

 Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' kabla ya kuonyesha uzi huo mpya alitangaza kuingia mkataba na kampuni ya A1 Production Limited ambao wanatengeneza kinywaji cha MO energy. 

 "Tumeingia mkataba na tunawakaribisha makampuni mengine kuja kufanya uwekezaji katika timu yetu," alisema Try Again. 

 "Fedha hizi ambazo tumepata kutoka kwa udhamini wa A1 tunazipeleka moja kwa moja katika uwanja wetu wa pale Bunju na habari njema ni kwamba tumekubaliana na muwekezaji Mohammed Dewji 'MO' ambaye ataweka pesa na mara moja tunaanza ujenzi," alisema Try Again. 

 Mkurugenzi wa A1 Production Limited, Mwanasara Sudi alisema wameingia mkataba wa mwaka mmoja kama utakwenda vizuri wataongeza. 

"Thamani ya mkataba wetu itakuwa Sh 250 Milioni na tunaimani kubwa tutapata matangazo ya kutosha kwani Simba ni sehemu kubwa ya matangazo hapa nchini," alisema Sudi. 

"Tulikuwa tukapata zaidi Sh 200 Milioni kwa msimu huku kukiwa na wapigaji wengi sasa tumeziba mianya hiyo kwa kiasi kubwa nadhani tutapata zaidi ya Sh 300 kwa msimu huu," alisema Sudi. 

 Katika hatua nyingine Afisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema klabu hiyo imeiingia na mkataba wa muda mfupi kwa ajili ya toleo maalumu siku ya Jumatano ya kampuni ya TSN ambao wanazalisha magazeti ya serikali. 

"Simba rasmi itazindua gazeti lake la (Simba Nguvu Moja) ambalo lilipanguliwa siku ya Jumatano na taarifa zote za klabu zitakuwa zikipatikana humo kwa wiki litatoka mara moja siku ya Jumamosi na litauzwa kwa Sh 500 tu," alisema Manara. 

"Hakutakuwa na magazeti yale ambayo yalitumika kwa jina la Simba tunaimani kama Uongozi hayatakuwepo tena na litakuwa hili tu ambalo litakuwa ni chanzo cha kipato kwa timu, " alisema Manara. 

"Tunaomba wapenzi na wanachama wa Simba kununua jezi zao ambazo si zile feki na zitauzwa sehemu maalumu kwa Sh 25000 tu na zitaanza kuuzwa Jumanne saa kumi jioni kwa Dar Es Salaam na baada ya hapo zitakuwa nchi nzima," alisema Manara.