Simba yawapa dili wanachama wapya

Muktasari:

  • Ndio! Mapema leo Jumapili walifanya mkutano kuelezea mikakati mipya na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, lakini hapo kukaibuka dili lingine tamu zaidi.

WAKATI bado wakiendelea kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ghafla tu mabosi wa Simba wakaibuka na saprize nyingine kwa mashabiki na wanachama wao.

Ndio! Mapema leo Jumapili walifanya mkutano kuelezea mikakati mipya na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, lakini hapo kukaibuka dili lingine tamu zaidi.

Iko hivi. Uongozi wa Simba umetangaza fursa mpya kwa mashabiki ambao si wanachama kwamba, kuna nafasi 50,000 kwa wanaotaka kuwa sehemu ya umiliki wa mabingwa hao wa Msimbazi.

Simba imeuza asilimia 41 ya hisa zake kwa bilionea, Mohamed Dewji ‘MO’ na kubakiwa na hisa asilimia 51 ambazo zitamilikiwa na wanachama hivyo, kwa idadi ya walionao kwa sasa hawawezi kufikia lengo la kumiliki asilimia hizo za hisa.

Ndipo, Mwanasheria wa Simba, Evodius Mtawala akaeleza kuwa mpaka sasa wanachama waliopo ndani ya Simba wana hisa zenye thamani ya Sh4 bilioni huku kiasi kinachohitajika kikiwa ni Sh17 bilioni ambazo zitakwanda kufanya kupatikana kwa umiliki wa asilimia 51.

Hata hivyo, kwa wanachama wapya ambao watataka kujiunga na Simba kwa sasa watalazimika kuanza kwa kulipa kiasi cha Sh400,000 badala ya 20,000 ya awali.

"Tunahitaji wanachama wapya kama 50,000 ambao watatuwezesha kufikia lengo la umiliki wa asilimia 51 ya hisa. Lakini, wanachama wapya watatakiwa kilipia Sh 400,000 badala ya ile ya zamani ya Sh20,000 ili kuendana na kasi mpya,” alisema Mtawala.