Lipuli kusajili sita

Muktasari:

Alisema, wamefikia hatua nzuri ya usajili, lakini waliamua kuweka kando suala hilo na kuelekeza nguvu zao kwenye mechi hiyo ili wafanye vizuri baada ya kufungwa na Singida United, bao 1-0.

KOCHA wa Lipuli ya Iringa, Amri Said amesema, watasajili wachezaji sita kwenye dirisha dogo ambao watakuwa ni wakongwe na chipukizi, lakini watawaweka wazi mara tu baada ya kumaliza mchezo wao na Simba,  Jumapili hii kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Alisema, wamefikia hatua nzuri ya usajili, lakini waliamua kuweka kando suala hilo na kuelekeza nguvu zao kwenye mechi hiyo ili wafanye vizuri baada ya kufungwa na Singida United, bao 1-0.
"Baada ya kufungwa na Singida United, matarajio yetu makubwa yamehamia katika mechi yetu na Simba, angalau tuweze kupata pointi tatu za ugenini, zitakazotuweka kwenye nafasi nzuri ya msimamo wa ligi kuu,"alisema Amri, mchezaji wa zamani wa Simba.
Amri aliongeza kwa kusema, watasajili wachezaji sita chipukizi na wakongwe ambao wataongeza nguvu katika kikosi chao hasa kuelekea mzunguko wa pili.
"Mzunguko wa pili ni mgumu, lazima tujipange, kwani kunakuwa na mambo matatu,zipo timu zinazokuwa zinawania ubingwa, nafasi tatu za juu na zile zinazojinasua na kushuka daraja,"anasema.