Simba,yanasa,kiungo Mkenya

MABINGWA wapya wa Ligi Kuu Bara, Simba ndio kwanza wameshika kasi kusajili vifaa matata ili kuhakikisha msimu ujao wanatoa vipigo kama kawaida. Tayari wamenasa saini za washambuliaji watatu ambao ni Adam Salamba aliyetokea Lipuli ya Iringa, Marcel Kaheza (Majimaji) na Mohammed Rashid (Tanzania Prison).

Hata hivyo, Simba ambao watawakilisha Taifa katika michuano ya klabu Bingwa Afrika, wameanza mazungumzo na kiungo matata wa Gor Mahia ya Kenya, Francis Kahata.

Kahata, ambaye alitisha kwenye michuano ya SportPesa Super Cup iliyomalizika hivi karibuni na Gor Mahia kubeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo kwa kuichapa Simba mabao 2-0. Mwanaspoti linafahamu kuwa, Simba imedhamiria kumshusha kikosini mwake kiungo huyo ambaye inaelezwa kuwa Yanga ilikuwa ikimpigia hesabu kabla ya MO Dewji kuingia jumla kutaka kuinasa ya kiungo huyo.

Mwanaspoti linafahamu kuwa kwa sasa mazungumzo yameshika kasi kuhakikisha dili linakamilika kwa haraka.

Kahata, ambaye anatambulika uwanjani kutokana na rasta zake na kutumia mguu wa kushoto, pia ana uwezo wa kucheza winga zote pia akiimudu vyema namba 10.

Habari za uhakika ambazo Mwanasposti imezinasa ni kwamba, mabosi wa Simba wanaendelea na mazungumzo na wakala wa Kahata na kwamba, na kiungo huyo ametaka kwanza kuhakikishiwa mshahara wa Sh4 milioni kisha taratibu zingine zitaendelea.

Uhakika wa Simba kumnasa Kahata unatokana na ukweli kwamba, anamaliza mkataba wake na Gor Mahia mwezi Novemba, mwaka hu, na mpaka sasa hawajafikia mwafaka wa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Kenya na SportPesa.

Pamoja na Simba kujihakikishia kumnasa, Yanga hawajakata tamaa kwa kuwa ndio walioanza harakati za kusaka saini yake kimya kimya sanjari na straika wa Gor, Meddy Kagere.

Kwa sasa Yanga imeanza kurejesha matumaini ya kutunisha misuli kwenye usajili hivyo, Simba wamekuwa siriazi zaidi kuhakikisha wanamaliza dili hilo mapema.

“Tangu msimu uliopita tulikuwa tunamuangalia Kahata, lakini idadi ya wachezaji wa kigeni ndani ya kikosi chetu ilikuwa imefika mwisho hivyo tulimweka kiporo. Msimu huu tutakamilisha usajili wake mapema kwani, tunafahamu Yanga nao wanamuhitaji,” alisema kigogo mmoja wa Simba (Jina lake tunalo).

MSIKIE TRY AGAIN

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kwa sasa wameamua kuingia kazini kusuka kikosi cha maana ili kushindana na vigogo wengine Afrika. Alisema wanaifanyia kazi kwa vitendo kauli ya Rais Dk. John Magufuli ya kuwataka kukiimarisha kikosi chao ili kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Try Again alisema kwa uwekezaji ambao upo au unakuja kufanyika ndani ya Simba wana uwezo wa kusajili mchezaji yoyote kutoka Afrika, ambaye atakuwa anahitajika na benchi la ufundi.

“Tutaimarisha timu yetu ili kuwa imara na kushindana na timu yoyote ambayo tutakutana nayo, tutaendelea kufanya usajili makini wa mchezaji yoyote ambaye tutakuwa tunamuhitaji,” alisema. “Naimani ndani ya miaka 5-10 tutakuwa na timu imara ambayo imekamilika ndani yaani katika benchi la ufundi na wachezaji wazuri na hata uwekezaji nje ya uwanja,” alisema Try Again.

KAHATA NI NANI

Alizaliwa Mei 4, 1992 mjini Ruiru katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya. Alianza soka lake kwa kucheza timu ya Vijana Thika United 2006 na baadaye alikwenda kukipiga Ravenna FC 2008 kwa mkopo. Baadaye alirejea Thika na kuanza kucheza kwenye kikosi cha wakubwa cha Thika United kuanzia mwaka 2008 hadoi 2015.

Alianza kuingia anga za soka la kimataifa kwa kujiunga na University of Pretoria mwaka 2010, ambako alikwenda kwa mkopo kisha akatua KF Tirana ya Albania mwaka 2014.

Akiwa na KF Tirana, alicheza mechi 16 na kupachika mabao matatu. Mwaka 2015, alirejea nchini Kenya na kujiunga na Gor Mahia, na tangu wakati huo amekuwa mchezaji tegemeo. Pia, ni mchezaji muhimu ndani ya timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, ambako mpaka sasa ameichezea mechi 21 na kupachika mabao mawili.