Simba yanasa kitasa Mkenya

UKISIKIA kutaka sifa ndiko huku. Mabosi Simba hawapoi kwani huku wakiendelea kumsaka kocha mpya wa kuchukua nafasi ya Mfaransa Pierre Lechantre, tayari washatua Kenya kumbeba beki na nahodha wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed.

Mbali ya kuingia vitani kusaka kocha, Kamati ya Usajili ya klabu hiyo inayoundwa na Mwekezaji, Mohammed Dewji ‘MO’, Kaimu Rais wao, Salim Abdallah ‘Try Again’ na vigogo wengine watatu (majina tunayo) wanaendelea kufanya yao kusuka kikosi hicho kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano mingine ikiwamo ya kimataifa.

Mabosi hao wameamua kumfuata beki wa kati wa Harambee Stars na aliyewahi kuwa nahodha wa Gor Mahia Musa Mohammed, ili aje kuchukua nafasi ya Juuko Murshid.

Mohammed aliyekuwa Albania akiichezea KF Tirana inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, anajiandaa kutua Msimbazi baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita na timu hiyo aliyojiunga nayo Januari mwaka huu.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinyaka zinasema kuwa nahodha msaidizi wa Harambee Stars alionwa na mabosi wa Simba kwenye michuano ya Cecafa yaliyofanyika Kenya na wenyeji kubeba taji mbele ya Zanzibar Heroes.

Inaelezwa kuwa Kamati hiyo ya usajili ya Simba licha ya kuanza mazungumzo ya awali na wakala wa beki huyo, Paul Augostino ‘Mendes’, lakini Mwanaspoti linafahamu pia nyota huyo anawindwa vikali na Kabwe Worriors inayoshishiriki Ligi Kuu ya Zambia.

Wakala Mendes amewaambia viongozi wa Simba kama kweli wamedhamiria kumtaka nyota huyo wafanye haraka kwani licha ya kutakiwa Zambia alizungumza pia na viongozi wa Singida United na Azam.

WASIKIE VIGOGO

Mjumbe mmoja wa Kamati ya Usajili ya Simba amelidokeza Mwanaspoti kuwa jina la Mohammed lipo katika orodha ya mabeki wanaowataka na kama wataafikiana naye atatua Msimbazi kuchukua nafasi ya Juuko anayetokea Uganda.

“Mpango wa kumtaka Mohammed upo na tulishafanya mazungumzo naye mapema, ila katika nafasi ya mabeki wa kati tunaowataka kuwaongeza yapo majina matatu na moja kati ya hilo linaweza kupita na tukamalizana naye,” alisema kigogo huyo.

“Wakala wake ametuambia ameongea na Singida, Azam lakini hatuna presha wala haraka Mohammed yupo katika mipango yetu ya ndani kabisa na jambo ambalo limetufanya kuwa kimya katika usajili ni kusaka kocha mpya kwanza,” alisisitiza kigogo huyo aliyeomba kuhifadhiwa majina.

Katibu wa Singida, Abdulrahman Sima alikiri kuongeza na wakala wa beki huyo wakiwa Kenya katika mashindano ya SportPesa na walifikia katika hatua nzuri ya makubaliano ya kumchukua.

“Kubwa ambalo limetufanya kuwa kimya katika kukamilisha usajili wa Mohammed tulifanya mabadiliko ya kocha na hatujajua kama atamuhitaji au atataka kubaki na wachezaji ambao amewakuta,” alisema.

“Tumekuwa na makosa mengi katika nafasi ya mabeki wa kati naimani tukimpata Mohammed kwa uzoefu aliokuwa nao anaweza kuongeza kitu, lakini hatutafanya lolote kuhusu yeye mpaka hapo benchi la ufundi litakaposema tumsajili au tuachane naye.”

Upande wa Azam kupitia Meneja wao, Philip Alando alisema: “Mawasiliano yalikuwepo kabla ya kumsajili Nicholas Wadada, ila baada ya kukamilisha usajili wa beki huyo Mganda, tumefunga zaezi zima la usajili na kama tutafanya basi itakuwa ni baada ya Kagame.”

MUSA MOHAMMED

Beki huyo anayemudu kutumia miguu yote kuanzisha mashambulizi, ana nguvu ya kushindana na washambuliaji wasumbufu na ni mahiri kwa kupiga pasi, alizaliwa Juni 6, 1991 Kenya na kwa sasa ana umri wa miaka 27.

Mbali ya kucheza nafasi ya beki wa kati, lakini Mohammed anamudu pia beki za pembeni na huwa mtamu zaidi akiachiwa acheze kwa uhuru kwa kuzalisha mashambulizi.

Kabla ya kwenda KF Tirana, alianza kucheza soka la ushindani mwaka 2010 akiwa Gor Mahia inayonolewa na Muingereza Dylan Kerr, huku akiichezea Harambee Stars tangu mwaka 2011 ambako mpaka sasa amefikisha michezo 25 na timu hiyo ya taifa lake.