Simba yamhamishia Niyonzima uzunguni

Friday August 11 2017HARUNA NIYONZIMA

HARUNA NIYONZIMA 

By DORIS MALIYAGA

MARA baada ya kutua Simba, matajiri wa kikosi hicho, wamemuhamisha kiungo wao, Mnyarwanda Haruna Niyonzima kutoka Magomeni na kumtafutia nyumba Mikocheni anakoishi sasa na amewaahidi kazi tu.

Niyonzima alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga na atakutana nao katika Ngao ya Jamii Agosti 23. Kuhusu mchezo huo alisema kuwa hana wasiwasi  na anaukabidhi kwa Mungu.

Ameliambia Mwanaspoti, ametua Simba na kuwa jambo hilo alikuwa  rahisi kwake: “Si jambo rahisi kutoka Yanga na kwenda Simba lakini haya ni maisha tu, kitu ninachoweza kusema ni kuwaahidi mabosi wangu wapya wa Simba kuwa nitawafanyia kazi, kikubwa ni ushirikiano tu.”

“Naishukuru Yanga nimekaa nayo kwa kipindi kirefu takribani miaka sita, wakubaliane na maamuzi yangu, kama nilivyosema hii ni kazi tu,”alisema Niyonzima.

“Mechi ya Ngao ya Jamii na Yanga itakuwa mgumu kwa sababu ya ushindani lakini kwa nafasi yangu nimejiandaa kimwili na kisaikolojia kuhakikisha nakwenda nao sawa na mambo mengine namwachia Mungu kwa sababu ndiye anayepanga.

“Unapofanya maamuzi kama haya unakuatana na changamoto nyingi hasa kutoka kwa mashabiki, nitazikabili na hazitanisumbua lakini kwa wale waliokuwa wangu waendelee kuniunga mkono kwa sababu haya ni maisha tu,”alisema Niyonzima ambaye alipokuwa Yanga alikuwa kipenzi cha mashabiki ingawa kila walipokutana na Simba walimpigia kelele kuwa ana mapenzi na Wekundu hao wa Msimbazi.

Awali, Niyonzima alikuwa anaishi maeneo ya Magomeni jijini Dar es Salaam pamoja na familia yake, lakini baada ya kutua Simba tu, mabosi wake wakamtafutia nyumba Mikocheni ambako kuna gharama zaidi na mambo mengi yamekaa kishua.

AMUAHIDI KAZIMOTO ZAWADI

Niyonzima alicheza kwa dakika 45 za kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Rayons Sports ya Rwanda ya utambulisho kwenye sherehe za Simba Day akiwa na jezi namba nane. 

Ni Mwinyi Kazimoto ndiyealimpa heshima ya namba nane. Kazimoto alimvulia jezi hiyo aliyokuwa anaivaa ndani ya kikosi hicho na yeye kuchukua 24, kitendo ambacho kimemfanya Mnyarwanda huyo amuahidi zawadi nono ikiwa ni ukumbusho kwake.

“Namba nane ndiyo jezi ninayovaa ninapokuwa katika timu yoyote, sijawahi kucheza nikiwa na namba nyingine na hivyo kwa kitendo ambacho Kazimoto amekifanya naweza kusema ni heshima kubwa na mimi namwahidi zawadi nzuri ikiwa ni ukumbusho wake,” alisema mchezaji huyo ambaye kwa sasa anaanza kuzoea uzi mwekundu.