Simba yaleta kiungo Mzambia

Muktasari:

  • Juzi tu wamemtambulisha kocha mpya, Mbelgiji Patrick Aussems, tena kwenye hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini kama haitoshi jana Ijumaa wamemleta kwa usiri mkubwa kiungo matata wa Zambia, Chama Clatous.

WANACHOFANYA Simba kwa sasa ni sifa tu unaambiwa kwani wakati watani wao wa jadi wakilia njaa, wenyewe wameendelea kufungua pochi na kushusha mastaa wa kimataifa.

Juzi tu wamemtambulisha kocha mpya, Mbelgiji Patrick Aussems, tena kwenye hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini kama haitoshi jana Ijumaa wamemleta kwa usiri mkubwa kiungo matata wa Zambia, Chama Clatous.

Habari ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba kwa kiungo huyo, timu pinzani zitapata tabu sana uwanjani.

Chama aliwasili jana na akaungana na wenzake kufanyiwa uchunguzi wa afya pale Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na muda wowote atasaini mkataba ili kuchukua nafasi ya kiungo Mkongomani, Fabrice Mugeni, ambaye alishindwa kusaini mkataba na Simba kutokana na kubanwa na masharti ya mkataba kwenye klabu yake ya Kiyovu.

Kama unavyojua kwa sasa suala la pesa si tatizo ndani ya Simba, mabosi wakapanda mwewe hadi Zambia na kuvamia kambi ya Lusaka Dynamos na kumchomoa Chama.

Chama anatajwa kuwa mmoja wa viungo bora kwa sasa kwenye Ligi Kuu Zambia na amewahi kuzichezea pia klabu za Nchanga Rangers na Zesco United.

Usajili wake ni pendekezo la kigogo mmoja wa Kamati ya Usajili baada ya kuzungumza na kocha Masoud Djuma, ambaye alisema anamfahamu kiungo huyo. Chama ana uwezo wa kufunga, kupiga pasi ndefu na fupi ambapo, anatumia nguvu na akili nyingi katika kukabiliana na mabeki wagumu kama Kelvin Yondani au Agrey Morrsi. Anaweza kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa Chama amebakiza miezi sita kwenye mkataba wake wa sasa na Simba inaweza kununua sehemu iliyobaki ili kukamilisha mchakato huo.

Kwa msimu huu, ameichezea timu yake hiyo mechi 11 na kupachika mabao matatu na ametajwa kuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachosafiri kwenda Uturuki kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

Mwanaspoti ambalo limekutana na kiungo huyo mshambuliaji akiwa kwenye msafara wa wachezaji wa Simba waliokwenda kufanyiwa vipimo wakiongoziwa na Mratibu wa timu, Abbas Suleiman, hakutaka kuzungumza lolote huku akisema watu sahihi wa kuzungumza kuhusu yeye ni mabosi wa Simba.

WAPIMWA AFYA

Jana, wagonjwa na watu waliokwenda kuwaona ndugu na jamaa zao walibaki macho kodo wakati mastaa wa Simba walipofika kwenye Taasisi ya Jakaya Kikwete kupimwa afya.

Simba imeamua kuendesha mambo yake kisasa zaidi, ambapo wachezaji wote walikwenda hospitalini hapo kufanyiwa vipimo, utaratibu ambao hata wenyewe wameupa tano.

Kiungo wa kimataifa wa Ghana, James Kotei, alisema utaratibu huo ni mzuri kwa sababu mchezaji anakuwa anajua afya yake mapema.

“Hili ni jambo zuri na timu zote wanatakiwa kuiga utaratibu wa Simba, hata nilipokuwa nyumbani Ghana tulikuwa tunafanya pia kitu kama hiki,” alisema.

Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘ Tshabalala’, alisema upimaji wa afya kwa wachezaji ni jambo la msingi na kwamba, inasaidia kuwaepusha na madhara uwanjani.

DOKTA AFUNGUKA

Daktari wa Simba, Yassin Gembe, ameliambia Mwanaspoti kuwa vipimo vya aina hiyo hufanyika kila mwaka na lengo kuu ni kujua afya za wachezaji.

“Huwezi kumsajili mchezaji kama hajafanyiwa vipimo kwa sababu katika fomu ya usajili lazima ujaze sehemu ya vipimo, kwa hiyo huu ni utaratibu wetu tuliojiwekea,” alisema.