Simba yajitosa vita ya matajiri

Muktasari:

>>Ni hivi. Nguvu ya pesa sasa imehamia ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ ameingia vitani 

MISIMU michache iliyopita, Simba ilikuwa ikiburuzwa kwa kila hali na watani zao Yanga iliyokuwa chini ya bilionea, Yusuf Manji huku Azam FC inayomilikiwa na bilionea mwingine, Said Salim Bakhresa, nayo ikiwabana mbavu.

Kitendo cha Simba kuburuzwa na wapinzani wake, kilisababisha watani zao Yanga kuwabatiza majina lukuki likiwamo la Wa Mchangani, hasa kutokana na kupitisha karibu miaka mitano bila kunyakua taji la Ligi Kuu Bara./

Simba ilinyakua taji la ligi hiyo mara ya mwisho mwaka 2012 na tangu hapo imeshuhudia Azam ikibeba taji mara moja na Yanga ikibeba taji hilo mara nne.

Hata hivyo kwa sasa mashabiki wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara wanatabasamu baada ya kung’amua kuwa klabu yao imeingia kwenye vita ya matajiri bila kutarajiwa huku watani zao wakihenya kujikwamua.

Ni hivi. Nguvu ya pesa sasa imehamia ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ ameingia vitani akitarajiwa kutumia nguvu ya ziada kuvunja ufalme wa bilionea mwenzie, Said Salim Bakhresa, mmiliki wa Azam.

MO ameshinda zabuni ya kumiliki asilimia 50 ya hisa za Simba kwa Sh20 bilioni, japo Serikali imesisitiza kuwa mwekezaji anapaswa kumiliki asilimia 49 tu.

Wakati MO akisubiri taratibu nyingine za kiofisi zikamilike ili aweze kupewa timu, Bakhresa ndiye kinara kwa sasa kwa timu za Ligi Kuu kuanzia kwenye mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na miundombinu ya klabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Azam ni kwamba, bajeti ya klabu hiyo kwa maana ya kulipa mishahara watumishi wote, kuendesha timu za vijana na taratibu nyingine kwa mwezi pale Chamazi inafikia Sh350,400 kwa mwezi.

Awali kabla ya mpango wa kubana matumizi ulioanzishwa na Mtendaji Mkuu, Abdul Mohammed, Azam ilikuwa ikitumia kati ya ShSh500 milioni hadin 600 milioni kwa mwezi na kuwa klabu yenye matumizi makubwa zaidi Afrika Mashariki.

Azam kwa sasa imeajiri wafanyakazi zaidi ya 150 ili kukidhi mahitaji ya kuendesha timu zao zote, kuanzia zile za vijana hadi ya wakubwa.

Azam pia ndiyo timu inayoongoza kwa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, ambapo kwa mwezi wanalipa zaidi  ya Sh160 milioni.

Yanga inatajwa kulipa mishahara ya Sh120 milioni, huku Simba ikipanda hadi nafasi ya pili kwa kulipa Sh125 milioni kwa mwezi. Simba imetua nafasi hiyo hata kabla ya MO hajapewa timu na inatabiriwa akipewa Simba itatisha.

Azam ya Bakhresa pia ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu yenye timu za vijana chini ya miaka 13, 15, 17 na 20, lakini tayari MO tayari ameahidi kutengeneza timu hizo ili kuifanya Simba iwe ya kisasa zaidi.

“Tunataka kuwa na timu imara za vijana vitakazozalisha vipaji, tutajenga akademi ambayo itakuwa kama chuo cha kuzalisha wachezaji wa kuuza ndani na nje ya nchi,” alisema MO mara tu baada ya kutangazwa mshindi.

MIUNDOMBINU

MO ambaye kibiashara anashindana pia na Bakhresa, atalazimika kuharakisha mipango yake ili kufikia ufalme wa mwenzake ambaye tayari amejipambanua Ligi Kuu.

Azam ya Bakhresa inamiliki uwanja wa mazoezi na mechi, hosteli, gym na miundombinu mingine ya soka katika eneo la Chamazi.

Miundombinu hiyo inakadiriwa kufikia zaidi ya Sh5 bilioni ambayo ni sawa na robo ya fedha za MO alizoweka Simba.

Azam kwa sasa ndiyo klabu pekee inayomiliki miundombinu hiyo miongoni mwa timu za Ligi Kuu, lakini MO amefichua kuwa ataweka mpunga wa maana kuanzia kwenye benchi la ufundi mpaka fungu la usajili huku akiahidi kujenga viwanja viwili fasta, kitu kinachowafanya Wana Simba kutabasamu kwa maana wanaona wakati wao wa kutamba ndio huu.