Simba yaitega Yanga

Muktasari:

  • Wadau wa soka wakiwamo nyota wa zamani wa kimataifa wametoa maoni yao juu ya tofauti za maandalizi ya timu hizo wakidai inaweza kuifanya Ligi Kuu Bara msimu huu kupungua msisimko licha ya ligi hiyo kuwa na klabu 20.

SIMBA tayari ipo nchini Uturuki ikianza kambi yao ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, lakini kitendo cha timu hiyo kunawiri kwa sasa kimekuwa ni mtego kwa watani zao Yanga, ambao wameyumba kwa siku za karibuni.

Wadau wa soka wakiwamo nyota wa zamani wa kimataifa wametoa maoni yao juu ya tofauti za maandalizi ya timu hizo wakidai inaweza kuifanya Ligi Kuu Bara msimu huu kupungua msisimko licha ya ligi hiyo kuwa na klabu 20.

Abeid Kasabalala, nyota wa zamani wa Mecco, Abdallah Kibadeni aliyewahi kung’ara na Simba na Taifa Stars na Kocha wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’, walisema kwa nyakati tofauti kuwa ligi ipo shakani.

Kasabalala alisema kuwa ubora kwa Simba na Yanga unaongeza msisimko wa soka nchini, hivyo kitendo cha Simba kung’ara na Yanga kudorora kitayumbisha ligi ya msimu ujao kwani mashabiki wachache watajitokeza viwanjani.

“Ingawa kwa Simba inaweza kuwa na kicheko kuyumba kwa Yanga, lakini kiuhalisia huu ni mtego kwani ligi itapoa, mfano tumeona kwenye Kombe la Kagame, kujitoa kwa Yanga kuliondoa shamrashamra zilizozoeleka,” alisema Kasabalala.

“Utani wa klabu hizi kongwe unaleta amsha amsha kwenye ligi, lakini kwa sasa ni kama Simba imeitega Yanga katika kushawishi mashabiki kujitokeza uwanjani kuziunga timu hizo na Ligi Kuu kwa ujumla.”

Bilo kwa upande wake alisema; “Kiukweli timu zote zinazoshiriki VPL, zinapaswa kujiandaa vilivyo ndipo ushindani unaweza ukavuta mashabiki kufuatilia soka, ila kwa desturi msisimko mkubwa unatoka kwa mashabiki wa Simba na Yanga.”

Naye Kibadeni alisema timu za ligi zinapaswa kufanya usajili na maandalizi ya kutosha, lakini kwa sasa Yanga ipo mtegoni kwani inaonekana kuyumba, huku wenzao wakitamba, hili linaweza kuwa tatizo na kupunguza msisimko.”

Simba ilipaa alfajiri ya jana kwenda Uturuki kuweka kambi ikiwa na Kocha Mkuu wao mpya, Patrick Aussems, ilihali Yanga wakitaabika kuwabembeleza nyota wao waliokuwa kwenye mgomo wakijiandaa mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia itakayopigwa Julai 29 katika Uwanja wa Taifa