Simba rekodi, Azam FC ubabe

Muktasari:

  • Timu hizo jioni ya leo zitapambana katika mchezo wa fainali utakaopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku Simba ikibebwa na rekodi tamu ya michuano hiyo na Azam wakibebwa na ubabe walionao tangu waanze kushiriki Kagame.

MASHABIKI wa soka wanataka kujua ni Simba ama Azam itakayobeba Kombe la Kagame 2018.

Timu hizo jioni ya leo zitapambana katika mchezo wa fainali utakaopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku Simba ikibebwa na rekodi tamu ya michuano hiyo na Azam wakibebwa na ubabe walionao tangu waanze kushiriki Kagame.

Simba ndio klabu iliyotwaa taji la michuano hiyo mara nyingi ikibeba mara sita, huku Azam ikishikilia rekodi ya kutofungwa kwenye michuano hiyo tangu mwaka 2015, ilipotwaa taji hilo bila kuruhusu hata bao moja.

Kabla ya fainali itakayopigwa saa 12 jioni, mapema mchana JKU ya Zanzibar na Gor Mahia ya Kenya zitacheza mchezo wa kusaka nafasi ya tatu pambano litakalochezwa saa 9 alasiri uwanjani hapo.

Rekodi zinaonyesha Simba imelibeba taji hilo mwaka 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, huku ikipoteza fainali tano hivyo leo itakuwa na kazi ya kufuta ukame wa kamati ya Kagame kama ilivyofanya katika Ligi Kuu Bara waliotwaa msimu uliopita.

Makocha wa timu zote wametamba kuelekea mchezo huo na Kocha Masoud Djuma wa Simba alikiri wanakazi kubwa kwa Azam, lakini wamejipanga kupata matokeo, akitegemea Meddie Kagere na wenzake kuendeleza moto wao.

“Mipango yetu ya kwanza nilikuwa kuwa bingwa ndio maana nimetenga muda kuwafuatilia wapinzani ili kujua mbinu gani za kuwapita na kuwazidi ili kuhakikisha tunawafunga na kuwa mabingwa.

“Nina imani tukichukua ubingwa itakuwa chachu kwetu kufanya vizuri katika Ligi na hata mashindano mengine ambayo yatakuwa mbele yetu msimu ujao, “ alisema Djuma.

Hata hivyo Kocha wa Azam, Hans Van Pluijm alisema Simba ni timu nzuri na mechi itakuwa ngumu kulingana na uwezo walionesha timu zote mbili ambazo zitacheza fainali leo, huku akiwa na kumbukumbu wa kubeba taji 2015 bila kupoteza.

“Ndio kwanza nimeingia katika timu ndio naweka mipango yangu katika kuijenga timu, mechi kama Simba ni kipimo sahihi kwetu tuna imani kubwa tutashinda lakini tunatambua pia mpira una matokeo matatu,” alisema.

Naye Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr alisema mechi yao na JKU itakuwa ngumu kutokana na kwamba walikuwa na malengo ya kuwa mabingwa lakini hayakutimia na huenda sababu kubwa ilikuwa wachezaji wake kutumika zaidi.

Kocha wa JKU, Hassan Ramadhani alisema anaomba waamuzi wa mechi ya leo wachezeshe vizuri si kama ilivyokuwa na Simba.