Simba kushusha mashine tatu

Muktasari:

  • Simba tayari imewasainisha mastraika watatu ambao ni Adam Salamba kutoka Lipuli, Mohammed Rashid kutoka Prisons pamoja na Marcel Kaheza kutoka Majimaji ya Songea.

Nakuru. Simba inaendelea na usajili wake kimya kimya na sasa imeweka wazi kuwa itasajili wachezaji watatu wa kigeni.


Simba tayari imewasainisha mastraika watatu ambao ni Adam Salamba kutoka Lipuli, Mohammed Rashid kutoka Prisons pamoja na Marcel Kaheza kutoka Majimaji ya Songea.


Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Tryagain’ amefichua kuwa wataleta wachezaji tofauti wa kigeni kwa ajili ya kufanya majaribio, lakini lengo lao ni kupata watatu tu.


Rais huyo alisema wanaangalia programu za kocha wao zilivyo ndipo wawashushe nyota hao wa kigeni kwaajili ya majaribio, hasa baada ya kubaini kuwa unaweza kusajili mchezaji mzuri na bado akashindwa kufiti kwenye timu.


Kiongozi huyo wa juu zaidi ndani ya Simba alisema wanahitaji beki mmoja wa kati, kiungo mmoja na straika hivyo wataleta wachezaji wengi ili kupata waliobora ambao watajiunga na timu yao.


“Tutaleta wachezaji wa majaribio hapa, watakuja wengi, wanaweza kufika hatua 10, lakini lengo letu ni kusajili watatu,” aisema Tryagain.


“Lengo letu ni kuwa na timu imara msimu ujao. Tumebaini kuwa unaweza kwenda kumsajili mchezaji mzuri nje lakini akashindwa kufiti kwenye mfumo wa timu, awamu hii hatutaki hilo litokee.


“Nitakaa na kocha kuona program zake zimekaaje ili tuone hao wachezaji watakuja lini. Kama mambo yatakwenda vizuri wanaweza kuanza kuja kabla ya michuano ya Kagame, bado tuna muda wa kutosha kujenga timu imara,” alisema Rais huyo.