Simba kuimaliza Ndanda FC kwa staili ile ile!

Muktasari:

  • Simba itaondoka kesho Alhamisi kwa usafiri wa ndege ukiwa ni msafara wa wachezaji 20, pamoja na benchi la ufundi lililo chini ya Kocha Patrick Aussems tayari kwa mchezo wao wa Jumamosi hii na Ndanda, utakaopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Dar es Salaam. Kikosi cha Simba kimeendelea na mazoezi yake leo Jumatano katika Uwanja wa Boko Veterans lakini kitu ambacho Ndanda FC wanatakiwa kukijua, staili itakayowamaliza ni mipira ya krosi.

Simba itaondoka kesho Alhamisi kwa usafiri wa ndege ukiwa ni msafara wa wachezaji 20, pamoja na benchi la ufundi lililo chini ya Kocha Patrick Aussems tayari kwa mchezo wao wa Jumamosi hii na Ndanda, utakaopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

 

Katika mazoezi ya Simba waliyofanya katika uwanja huo wenye nyasi asili kama Nangwanda, yalikuwa ni mbinu zaidi hasa katika kutafuta bao wakati wa kushambulia.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alikuwa anataka mawinga wote kulia na kushoto pamoja na mabeki wote wa pembeni kupiga krosi.

 

Wakati mabeki hao na mawinga wakipiga krosi hizo, kazi ya mastraika wa Simba ni kufunga tu na katika hilo hawakufanya mzaha kabisa.

 

Kila krosi iliyopigwa, Mnyarwanda Meddie Kagere, Emmanuel Okwi raia wa Uganda, Adam Salamba na Mohammed Rashid 'Mo Rashid', walikuwa wakiwatesa makipa kila ilipopigwa, ilikuwa bao.

 

Staili hiyo si ngeni ndani ya kikosi hicho, Simba wamekuwa wakiitumia mara kwa mara hasa kocha huyo Mbelgiji aliyechukua mikoba ya Mfaransa Pierre Lechantre.

Makipa waliocheza wakati wa zoezi hilo wakipishana ni Deogratious Munishi 'Dida', Said Mohamed 'Nduda' na Aishi Manula.

 

"Tutatumia zaidi mbinu katika kupiga krosi kutokana aina ya uwanja ambao tutatumia katika mechi ya Ndanda, " alisema.

"Mazoezihaya ambayo ya kimbinu tuliyoyafanya hapa ndio tutawatumia na kucheza kwa aina hii katika mechi, " alisema Aussems.