MAONI YA MHARIRI: Simba imeonyesha njia, klabu nyingine zikubali kubadilika

BAADA ya vikwazo vya hapa na pale hatimaye klabu ya Simba imeandika historia ya kwanza nchini kuachana na mfumo wa kizamani na kuendeshwa kisasa.

Simba imebadili mfumo wake wa uendeshwaji kutoka ule wa wanachama na kuingia katika mfumo wa hisa, baada ya Jumapili iliyopita bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji kutangazwa kuwa mwekezaji wa klabu hiyo.

MO Dewji amepewa Simba kwa hisa za Sh 20 bilioni ikiwa ni asilimia 50, japo Serikali inasisitiza hisa hizo zinapaswa kuwa asilimia 49 na zilizobaki zimilikiwe na wanachama.

Hatua iliyofikiwa na Simba ni ya kupongezwa kwa vile kwa dunia ya sasa mfumo wa uendeshaji wa klabu kwa njia ya wanachama umepitwa na wakati na huzitia klabu umaskini.

Hakuna ubishi kuwa klabu kubwa na kongwe za Simba na Yanga zina mtaji mkubwa wa wanachama na mashabiki ndani na nje ya nchi, lakini ni tegemezi wa mifuko ya watu binafsi.

Klabu hizo zimekuwa ombaomba na kuwanufaisha baadhi ya watu hususani viongozi badala ya kujinufaisha zenyewe katika umri wao wa miaka zaidi ya 80 tangu zilipoasisiwa miaka ya 1930.

Yanga walikuwa wa kwanza kushtuka tangu enzi za uongozi wa Katibu Mkuu wake marehemu George ‘Castrol’ Mpondela mwaka 1998 kwa kutaka kuigeuza kuwa kampuni. Baadaye alikuja Tarimba Abbas lakini mchakato ulikwama kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa mashabiki wa soka wanaokumbuka, mipango na mchakato huo uliisababishia Yanga na mgawanyiko mkubwa wa makundi ya Yanga Kampuni, Yanga Asili na Yanga Bomba.

Wanachama wasiopenda mabadiliko na wanaoishi wakiitegemea Yanga kupata masilahi waliupinga mfumo huo na hata hivi karibuni bilionea Yusuf Manji alipotaka kukodishwa timu na nembo ya klabu aliwekewa vikwazo.

Ila kwa vile Simba imefanikisha kilichowashinda watani zao, ni wazi hata wale wasiopenda mabadiliko ndani ya Yanga, sasa watalegeza misimamo yao na kuruhusu mfumo huo wa kisasa. Bahati nzuri uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umetangaza kufuata nyayo za Simba kwa kuitisha mkutano na wanachama wao, ili kieleweke.

Yanga imeyumba kwa sasa kiuchumi kwa vile aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wao Yusuf Manji alijiondoa kutokana na misukosuko aliyoipata kutoka serikalini, kiasi klabu ikakosa mtu wa kuipiga tafu kifedha.

Hali hiyo ni kama iliyokuwa nayo Simba miaka ya nyuma mara baada ya kukosa mfadhili na kuishia kutegemea mifuko ya watu.

Hii ni aibu kwa klabu kubwa zenye umri wa karibu nusu karne kuendelea kutegemea mifuko ya watu wakati zina hazina ya wanachama na mashabiki lukuki kila kona ya nchi.

Ni aibu kwa klabu kubwa kama hizo zenye majengo na vitega uchumi, zikiwa hakuishi zina hata viwanja vya mazoezi na zikiishi maisha ya omba omba yanayosababishwa na mfumo wa uendeshaji, kitu ambacho Simba imeukataa kwa sasa.

Kwa kuwa Simba imeonyesha mfano kwa wengine kwa kukubali kuingia kwenye mabadiliko, ni wazi tunatarajia mchakato wa Yanga utaleta tija kwa wanachama wao kuridhia mabadiliko ili kuifanya kampuni kama walivyopanga mapema mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Sio Yanga na Simba tu, bali hata klabu zote zinazoendeshwa kwa mfumo huo wa ujima zinapaswa kuamka na kubadilisha mifumo wa uendeshaji kwa kuruhusu wawekezaji ili kujikwamua kiuchumi.

Klabu kama za Coastal Union, Africans Sports, Toto Africans, Majimaji na nyingine zinapaswa kufuata nyayo za kubadilisha mfumo wa klabu zao kuwa wa kisasa.

Soka la zama hili la dunia ya sasa ni biashara inayoendeshwa kwa kutumia mamilioni ya fedha. Wachezaji wanasajiliwa kwa fedha nyingi, makocha wanaajiriwa na kulipwa mamilioni ya fedha na hata uendeshaji wa timu katika ligi ni fedha pia. Leo baadhi ya nyota wa Yanga wanaidengulia timu kwa kuwa tu klabu imeshindwa kukidhi mahitaji yao ya kimakubaliano ya kifedha. Ndivyo ambavyo Simba na klabu nyingine siku za nyuma zilivyokuwa zikipata tamu kwa nyota wao. Klabu zinazoendeshwa kizamani, lazima zibadilike na kuingia kwenye mfumo wa kisasa kama walivyofanya Simba. Wakubali wawekezaji waingia kuzifanya klabu zao kuendeshwa kisasa.