Mogella: Nisingemuondoa Mayanja

Muktasari:

  • Mganda huyo ameondoka Simba kutokana na matatizo ya kifamilia

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella “Golden Boy’ amewaambia viongozi wa klabu hiyo kama angekuwa na mamlaka angembakisha na kumpa ukocha mkuu Jackson Mayanja na kumtimua Joseph Omog.

Mganda Mayanja amevunja mkataba wake na Simba Jumatano iliyopita kwa kile alichodai ni matatizo ya kifamilia na tayari uongozi wa klabu umeziba pengo lake kwa kumchukua Mrundi Djuma Masoud.

Akizungumza na Mwanaspoti.co.tz, Mogella alisema Mayanja katika maisha yake ya kucheza ana historia kubwa ndiyo maana aliweza kakaa El Masry ndani ya miaka mitatu, wale watu hawawezi kumvumilia mchezaji mzigo ukiona hivyo alikuwa anajua kweli kweli, laiti ningekuwa kiongozi ningemng'ang'ania kwa vyovyote ili abaki na timu.

"Namfahamu vizuri namna ambavyo anaupenda mpira mwaka 1984, tulienda kucheza na timu yao ya taifa ya Uganda, tulishinda mabao 3-1, nilifunga mawili nakumbuka, marehemu Selestine Skinde alifunga bao la tatu, Mayanja alikuwa nyuma ya gori lao, tulipomaliza tu alinidaka kutamani kufahamu mafanikio yangu, alikuwa ni mdogo wakati huo," alisema Golden Boy.

Mogella alisema mchezaji asiyeridhika na anachokifanya kwa sasa, anayependa kujifunza kwa mwingine, atakuwa amehuzunika kuondoka kwa kocha huyo na kwa sababu ya maisha lazima ifikie hatua kila mtu ajue lake.