Simba iliwaza kombe,Kagera Sugar kutibua

Muktasari:

  • Ndio, Simba iliendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kuzidi kujikusanyia pointi za kutosha licha ya kuwa tayari ni mabingwa wapya.

BAO la dakika 23 la beki kiraka, Shomary Kapombe lilimaliza mchezo baina ya Simba na Singida United, uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Namfua mjini hapa.

Ndio, Simba iliendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kuzidi kujikusanyia pointi za kutosha licha ya kuwa tayari ni mabingwa wapya.

Mwanaspoti lililoweka kambi mjini Singida takribani siku nne, linakuletea baadhi ya mambo yaliyojitokeza kabla na baada ya mchezo huo uliosisimua mashabiki.

VYUMBA VYA WAGENI ViMEJAA

Alhamisi iliyokuwa siku ya kwanza kwa Mwanaspoti lilipotimba mjini Singida kufuatilia kila kinachojiri, lilikuta nyumba nyingi za wageni zimejaa na kwa taarifa tu ni kwamba, haijawahi kutokea hali kama hiyo katika mechi zote za Singida msimu huu.

Siku zote nne, nyumba nyingi za wageni zilisheheni mashabiki wa Simba ambao, walitoka Dar es Salaam na kuja kwa wingi mkoani hapa kushuhudia mechi hiyo.

James Orenel ni mmoja kati ya wahudumu katika nyumba za wageni, alisema haijawahi kutokea Singida ikakusanya mashabiki wengi wa soka kama ilivyokuwa kuelekea mechi ya Singida United na Simba.

“Katika kuelekea mechi hii tumefanya kweli biashara kwani, hoteli zetu hapa Singida nyingi zilijaa mashabiki wa Simba jambo ambalo tunaomba kujitokeza tena msimu ujao,” alisema Orenel.

BIASHARA, VYAKULA USIPIME

Kama kawaida kunapokuwa na mechi ambazo zinazikutanisha timu kongwe za Simba na Yanga kunakuwa na fursa nyingi zinazopatikana.

Hapa Singida kwanza kutokana na wingi wa mashabiki wa Simba ambao, walifurika kutoka Dar es Salaam, kumekuwa na biashara nyingi zikifanyika mojawapo ikiwa ile ya kuuza jezi ambazo zilikiwa na maandishi yaliyoandikwa Simba Bingwa 2017-18.

Biashara nyingine zilikiwa zile ndogondogo kwa Wamachinga, kuuza majaketi, soksi na vingine vingi hii yote kutokana na hali ya hewa ya hapa maana ni baridi kwelikweli.

Wauza vyakula nao walifaidika kutokana wingi wa mashabiki kufurahia huduma hiyo na chakula kilichoingiza fedha nyingi ni kuku wa kienyeji.

BODABODA NAO FRESHI

Ukiachana na usafiri walioutumia mashabiki wengi wakati wa kuja na kuondoka Singida usafiri wa ndani yaani bodaboda zilikuwa zikipishana kubeba watu.

Katika hali ya kawaida hapa Singida bodaboda ndio usafiri ambao ulikuwa bize muda wote, lakini ulikuwa sio wa gharama kubwa tofauti na ilivyokuwa kama Dar es Salaam.

MECHI ILIVYOKUWA

Kabla ya mechi kuanza mashabiki wengi wa Simba walifurika uwanjani kuanzia saa 4:00 asubuhi wakishangilia mwanzo mwisho, japo wale wa Singida nao hawakuwa nyuma katika kuishangilia timu yao jaopo ilipoteza. Singida ilipowasili saa 8:30, Namfua lilipigwa shangwe la kufa mtu ingawa Simba ilipowasili saa 9:00, uwanjani mzima ulilipuka kwa shangwe la maana.

Simba ilipasha ikiwa na imevaa jezi zilizoandikwa Asante SportsPesa kwa nyuma, huku mbele zikiandikwa Simba bingwa 2017-18, na mara baada ya kumalizika walivua na kuwarushia mashabiki wao.

Kabla ya mechi hiyo kuanza wabunge ambao ni mashabiki wa Simba waliwasili uwanjani hapo kushuhudia timu yao iliyoibuka na ushindi.

KUMBI ZA STAREHE

Mara baada ya kumalizika mechi mashabiki walitawanyika kila mmoja anapopajua, lakini usiku katika kumbi mbili za starehe yaani Sky Line na Ranbow Night Club kulisheheni watu waliokuwa wakila bata. Kwa kifupi mambo yalikuwa moto. Mbali ya kuwepo mashabiki katika kumbi hizo za starehe kulikuwa pia wachezaji, viongozi wa Singida United na Simba (majina tunayo), walishasahau kilichotokea ndani ya dakika 90 na wakasherehekea wote kwa pamoja.

MABASI YALIJAA

Jana Jumapili katika Kituo Kikuu cha Mabasi yanayoenda mkoani (Misuna), abiria waliokuwa wakirejea Dar es Salaam walikuwa wengi na magari yote yalijaa.

Mashabiki wengine walikosa nafasi katika mabasi na kufanya oda mapema kwa ajili ya kusafiri leo Jumatatu, ilimradi kila mmoja kurudi akikotoka wakiwa wamesuuzika na mziki mnene walioushuhudia pale Namfua, ambao umekuwa na maana kubwa kwa Simba.