Simba hii! haizuiliki wala haipigiki aisee

KIKOSI cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba kimetua usiku wa kuamkia jana Jumatatu wakitokea Uturuki, huku Kocha Mkuu Patrick Aussems akisisitiza sehemu kubwa ya kazi yake imeisha na kilichobaki ni vijana wake kufanya mambo.

Simba walitua kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki saa 8:45 usiku na mpaka walipotoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA karibu na alfajiri ikiwa ni wiki mbili tangu walipoweka kambi nchini humo.

Msafara huo wa Simba ulikuwa na nyota wote wakiongozwa na Kocha Aussems sambamba na Mulamu Nghambi ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya kupitisha mabadiliko ya klabu hiyo.

Mara baada ya kuwasili, Kocha Aussems alisema anadhani amekuja Simba katika muda mwafaka na kwa maandalizi waliyofanya ni dalili njema watafanya vizuri katika mashindano yote yaliyokuwa mbele yao.

Mbelgiji huyo aliyewamwagia sifa mabosi wa Simba kwa kuiandaa kambi hiyo, alisema amefundisha nchi nyingi, lakini maandalizi yao ya ligi huwa ya kawaida, tofauti na aliyofanya Simba na sasa ni kazi ya vijana kufanya mambo.

“Kwangu ninahisi kila nilichokuwa nataka kufanya katika maandalizi nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kilichobaki ni kuanza kuona wachezaji wakiyatekeleza haya kwa mafanikio makubwa kwani tuna kila sababu ya kufanya vizuri msimu huu.

“Wiki mbili za maandalizi ambazo tumekuwa Uturuki tumepata kila kitu ambacho tulikuwa tunahitaji kama benchi la ufundi na hata wachezaji na zaidi tulipata motisha kutoka kwa viongozi wa Simba, ingawa hawakuwepo lakini kwa upande wangu nilikuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara ili kufahamu kila tulichokuwa tunaendelea kukifanya,” alisema.

“Nimekutana na wachezaji wenye vipaji na uwezo wa kucheza soka na ambacho nilikuwa nawapatia kule ni mazoezi ya ufiti na mbinu nyingi ambazo tunakwenda kuzitumia katika mechi zetu na kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mechi.

“Siwezi kuwazungumzia wapinzani wowote ambao tutakutana nao katika ligi au michuano mingine, lakini kwa haya maandalizi tuliyofanya, kwangu ni ishara tosha ambao tutakutana nao wajiandae kweli kwani tuna kiu ya kuona tunapata matokeo mengi ya ushindi katika kila mechi,” aliongezea Aussems.

VIPI KOTOKO?

Simba kesho Jumatano wanavaana na Asante Kotoko ya Ghana katika mechi ya Tamasha la Simba Day watakayoitumia kutambulisha rasmi kikosi chao kipya na Kocha Aussems alipoulizwa kuhusu mchezo huo alisema; “Naifahamu Kotoko ni timu nzuri na naendelea kuifuatilia kabla ya kuwavaa, ila nadhani pia itakuwa mechi ya kipimo sahihi kwetu, kwani ni moja ya timu bora Afrika .”

Naye Nghambi aliyekuwa na mkewe alizungumza kwa kudai;

“Maandalizi yaliyofanyika ni mazuri na yenye tija na kuonyesha Wanasimba wote wana kiu ya kupata matokeo mazuri, kama uongozi umefanya jukumu lake la kuwapatia kila kitu wachezaji na benchi la ufundi na litaendelea kufanya hivyo na jukumu kubwa litabaki kwao.”

KAMBI YAVUNJWA

Wakati kikosi cha Simba kilipotua nchini, uongozi ulikuwa umeshaandaa basi kubwa la kubeba wachezaji kwa ajili ya kuwapeleka kambini Hoteli ya Serena, lakini gari hili liliondoka likiwa na wachezaji watano tu.

Wachezaji hao waliondoka na basi hilo ni nahodha msaidizi Mohammed Hussen ‘Tshabalala’, Adam Salamba, Asante Kwasi, James Kotei na Nicholas Gyan ambao nao kila mmoja alikuwa akienda nyumbani kwake.

“Wachezaji walitakiwa kwenda kambini wote, lakini nimeona vyema kuvunja ratiba hiyo hapa na nimetoa ruhusa ya siku mbili kila mchezaji aende nyumbani kwake kusalimia familia maana tutakuwa na ratiba nyingine ndefu,” alisema kocha mkuu.

“Nitaongea na viongozi ingawa wengine nimeshawaambia hili na tutafanya mazoezi leo (Jana) na kesho Jumanne katika Uwanja wa Uhuru na baada ya hapo ndio wataingia kambini.

“Wachezaji wakiwa kambini kwa muda mrefu wanakuwa wasumbufu kidogo ili kuhakikisha hilo halitokei ninadhani watakwenda kukaa na kusalimia familia zao kwa muda niliowapa nadhani unatosha,” alisema Aussems.

Hata hivyo, wakati tukienda mitamboni, inaelezwa Simba wameamua kuirejesha timu hiyo Sea Scape One, baada ya awali kukwama kwa kilichoelezwa KMC walikuwa wameweka kambi pale na kuwatibulia.