Simba Day yamgusa hadi Aunty Ezekiel unaambiwa

Wednesday August 8 2018

 

By THOMAS NG’ITU

LEO ndio Leo unaambiwa kwasababu wadau na wapenzi wa soka nchini walikuwa wakiisubiri siku hii ifike, ili waweze kuwaona wachezaji wao wapya wakitambulishwa katika Tamasha hili la Simba Day.

Kama kawaida ilivyo kwa upande wa Simba huwa wanaandaa tamasha lao maalumu kwa ajili ya kuwatambulisha nyota wao, leo watashuka dimbani kukipiga na Asante Kotoko kutoka Ghana hiyo yote ni kukipima kikosi chao kabla Ligi haijaanza.

Mwanaspoti liliwaangalia baadhi ya wasanii ambao ni mashabiki wa kalbu hiyo na kupiga nao stori mbili tatu wakizungumzia tamasha hili pamoja na jinsi ambavyo wanakiona kikosi chao.

MWANA FA

Msanii huyu alipata mpaka tuzo ya muhamasishaji bora katika mitandao ya kijamii wa klabu hiyo, mara kwa mara alikuwa akihusika kuandika posti ambazo zilikuwa zinapendwa na mashabiki wenzake wa Simba.

Awali ilitajwa kwamba nyota huyo hatokuwepo katika tamasha hilo, lakini alipozungumza na Mwanaspoti alisema kwamba atakuwepo katika tamasha hilo lakini hatopanda jukwaani kuimba.

“Kweli nilikuwa nisafiri lakini kilichotokea ni kwamba nilikuwa sijui nitaondoka saa ngapi ndio maana ikasemwa kwamba sitakuwepo nitakuwa Afrika Kusini, hata hivyo nitakuwepo nikiangalia timu yangu japo nitakuwa jukwaani.”

Akizungumzia kikosi chao cha msimu ujao baada ya kumaliza usajili, alisema kwamba ana uhakika mkubwa wa kutoka na matokeo kila anapokuwa anaenda kuangalia mpira hivi sasa.

“Kiukweli timu yetu hivi sasa kila nitakapokuwa naenda uwanjani nitakuwa na asilimia 85 za ushindi, kikosi kina wachezaji wazuri sana na ni kipana hizo asilimia zingine zinabaki kwasababu mpira unadunda,” alisema.

Mwana Fa aliongeza kwamba licha ya kwamba ana marafiki wengi wachezaji katika kikosi hicho, anawakubali sana wachezaji Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco, huku akiheshimu uwezo wa wachezaji wengine wa timu nzima jinsi ambavyo wanapambana katika kusaka matokeo.

AFANDE SELE

Mkali wa Rhymes ambaye alitamba na nyimbo zake kama Darubini kali, naye ni miongoni mwa mashabiki na vipenzi wa Simba.

Afande Sele alisema kwa maono yake jambo la Simba Day ni zuri, kwa sababu wachezaji wanakuwa wanatambulishwa na kila shabiki kufahamu.

“Sio kama ni jambo baya sana hilo ni zuri kwasababu watu watataka kuona namna ambavyo wachezaji wamekipata baada kukaa kambi uturuki,” alisema.

Akizungumzia kikosi chao kwa ujumla alisema kwamba usajili uliofanywa na muwekezaji Mohammed Dewji unaweza ukasaidia ndani ya Ligi Kuu Bara, lakini kwa upande wa Afrika bado anawasiwasi mkubwa.

“Kiukweli nina wasiwasi na aina ya wachezaji tuliowasajili kuelekea katika upande wa mechi za kimataifa, Mazembe walipokuwa wataka kombe la Afrika walikuwa wanasajili wachezaji wenye majina makubwa kutoka kila nchi na walifanikiwa wakachukua,” alisema.

Aliongeza kwamba kikosi chao ni kizuri na kinaweza kupata ushindi katika kila mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini kwa upande wa Kimataifa hana uhakika nacho kutokana na aina ya usajili walioufanya.

TUNDA MAN

Msanii mwenye sauti ya kipekee katika muziki, ambaye aliwahi kutamba na wimbo kama Starehe Gharama, alifunguka kwamba katika Tamsha la mwaka huu kuwaleta Asante Kotoko ni kipimo sahihi kwao.

“Asante Kotoko ni timu kubwa Afrika na kila mmoja anajua hili jambo, kwahiyo kujipima nao katika Tamasha hili kwasababu tutaona kabisa kiwango chetu kipo vipi,”.

Akizungumzia kikosi chao katika msimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, alisema kwamba kikosi chao ni kipana na kinaweza kikachukua ubingwa mapema mno.

“Kikosi chetu sasa hivi hakuna hata la kupoteza kiukweli, tunaweza tukachukua ubingwa mapema mno kwasababu wachezaji wetu ni wazuri halafu kikosi chetu ni kipana,”.

AUNT EZEKIEL

Msanii huyu wa Bongo Movie amefunguka kwamba mapenzi aliyokuwa nayo katika kikosi hicho cha Simba yamemfanya ashindwe hata kuhama na kwenda timu nyingine.

“Kiukweli naipenda Simba kadri siku zinavyozidi kwenda mbele kwasababu wanazidi kujidhatiti na kutengeneza kikosi chetu kuwa kizuri, acha niseme wazi kwamba sijawahi kufikiria kuhama Simba hata siku moja.” Aunt aliongeza kwamba Tamasha la Simba Day ni zuri kwa sababu wapenzi wa timu hiyo wote watapata fursa ya kuona wachezaji wao kwa mara ya kwanza wakiwa katika jezi. “Tamasha ni zuri kiukweli kwasababu mashabiki wanakuwa na hamu kubwa ya kutaka kuona namna ambavyo wachezaji wao wameiva kabla ya mechi zingine, hii ni siku ya furaha kwetu.”