Simba, Yanga zakalia kuti kavu

Friday January 12 2018

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Mafanikio na ubora wa timu za Singida United, Azam FC kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanaweka rehani nafasi za Simba na Yanga msimu huu.

Licha ya Singida kutolewa katika nusu fainali dhidi ya Azam, kiwango cha timu hizo kinatishia uwezekano wa Simba na Yanga kumaliza msimu bila kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu au Kombe la FA.

Ubora wa timu hizo unazifanya Simba na Yanga kukosa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa mwakani kwa mara ya kwanza katika historia ya soka nchini.

Rekodi zinaonyesha tangu zianzishwe, hakuna mwaka ambao Simba na Yanga zote zilikosa tiketi ya kushiriki mashindano ya ya kimataifa.

Yanga haina presha kwa sababu inashiriki Ligi Kuu na Kombe la FA inayotoa tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa kulinganisha na Simba.

Hali ni ngumu kwa Simba kwasababu nafasi pekee kwao kushiriki mashindano ya kimataifa itapatikana kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.

Kiwango Singida, Azam

Tathimini iliyofanywa na gazeti hili kupitia Kombe la Mapinduzi imebaini sababu nne zinazozipa nguvu Singida na Azam kuibuka wababe wa vita dhidi ya Yanga na Simba msimu huu.

Mapro

Wachezaji wa kigeni Singida United na Azam wametumia vyema fursa ya Kombe la Mapinduzi kujenga heshima kwenye timu zao kulinganisha na 'mapro' wa Simba na Yanga.

Beki wa kushoto wa Simgida United, Shaffiq Batambuze kutoka Uganda alitwaa zawadi ya mchezaji bora wa mechi mara tatu tofauti katika mechi walizocheza dhidi ya Mlandege, Yanga na dhidi ya Azam FC.

Nafasi ya vijana

Ingawa chipukizi wengi walicheza vyema katika Kombe la Mapinduzi, vijana wa Singida United na Azam zipo kwenye nafasi nzuri ya kuzisaidia timu zao.

Makocha wa timu hizo wamekuwa wakitoa nafasi kwa vijana kulinganisha na Simba, Yanga ambazo haziwatumii vijana wenye umri mdogo.