Simba, Yanga zagawana kambi

MECHI ya Ngao ya jamii ya Watani wa Jadi Simba na Yanga itapigwa Agosti 23 Uwanja wa Taifa, lakini katika kujiweka fiti klabu hizo zimegawana kambi.

Simba iliyokuwa Afrika Kusini inajiandaa kwenda kuweka kambi Morogoro, lakini kabla ya kuondoka Jumapili itaivaa Singida United jijini Dar es salaam.

Wakati Simba ikivaana na Singida kwenye Uwanja wa Taifa, watani zao watakuwa wapo visiwani Zanzibar kupimana ubavu na Mlandege kisha kwenda kujichimbia visiwani Pemba kupiga kambi.

Kabla ya kwenda Pemba, Yanga kwa wiki mbili walikuwa Morogoro wakijifua na kwenda kwao Zanzibar ni kama kuivamia ngome ya Simba.

Mkurugenzi wa Singida United Fasto Sanga alisema wanacheza na Simba Jumapili kama sehemu ya maandalizi yao ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

“Simba wanajianda kucheza na Yanga, na sisi tunajianda na Ligi Kuu, hivyo mchezo huo utakuwa mzuri wa kurekebisha makosa baada ya Yanga kutufunga mabao 3-2,” alisem Sanga.

Sanga pia alisema katika mechi hiyo ya Jumapili watamtumia straika wao mpya Michelle Katsvario kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Straika huyo ametua Singida kwa mkopo kuchukua nafasi ya Wisdom Mutesa aliyetemwa na mabosi wa matajiri hao wa Singida walipanda daraja.

Wakati Simba ikipimana ubavu na Singida, Yanga wenyewe Jumamosi watavaana na Ruvu Shooting kabla ya Jumapili kuwafuata Mlandege watakaoumana naoq Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mechi hiyo itapigwa siku moja kabla ya Yanga haijatua Pemba kupiga kambi ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba itakayopigwa Agosti 23.

Pia kambi hiyo itatumika kwa maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara msimu wa 2017-2018 itakayoanza Agosti 26 na uongozi wa Yanga umethibitisha hilo.