Simba, Yanga mmemsikia Pluijm anautaka ubingwa hatari

Muktasari:

  • Pluijm ametamba wachezaj wake wote wanaonekana kuwa na uchu wa mafanikio kitendo kinachomfanya ajiamini kila mechi inayokuja mbele yake baada ya ushindi wa mechi zake mbili za awali.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Pluijm amesema hana sababu za kumfanya ashindwe kutwaa ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chake.

Pluijm ametamba wachezaj wake wote wanaonekana kuwa na uchu wa mafanikio kitendo kinachomfanya ajiamini kila mechi inayokuja mbele yake baada ya ushindi wa mechi zake mbili za awali.

Kauli hiyo imetolewa na Pluijm baada ya kupata kikosi kingine katika michezo mitatu ya kirafiki waliyocheza kupisha timu ya Taifa 'Taifa Stars' iliyokuwa na kibarua cha mechi ya kufuzu fainali za AFCON dhidi ya Uganda iliyochezwa wikiendi iliyopita.

Pluijm alisema baadhi ya wachezaji wake waliitwa katika kikosi cha timu ya taifa na aliendelea na maandalizi kwaajili ya kukiandaa kikosi chake kwaajili ya michezo ya ligi iliyo mbele yao na kubainisha ameona vipaji vingi ambavyo vitamsaidia kufanya vizuri.

"Tumecheza michezo mitatu ya kirafiki tumetengeneza mabao manne na tumeruhusu mabao matatu naweza kusema safu ya ulinzi ilikosa umakini tatizo ambalo tayari nimeanza kulifanyia kazi kubwa nililoliona ni upana wa kikosi kilicho na uchu wa mafanikio naamini wachezaji wote wanatamani kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, nimewaona na nitalifanyia kazi," alisema.

Pluijm aliongeza kuwa safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Dany Lyanga katika michezo hiyo waliyocheza imeendelea kumpa changamoto zaidi kwani washambuliaji wengi wanaonekana kuwa na uchu wa kuzifumania nyavu na wamekuwa wakitendea haki nafasi wanazozitengeneza.

Anasema Lyanga ni mshambuliaji mzuri amejiunga Azam kwa lengo moja la kuhakikisha inafanya vizuri kwani anaonyesha anajua nini anakifanya akiwa uwanjani pia ni mchezaji ambaye anajua kucheza na akili za mabeki naamini ataisaidia sana timu hasa safu ya ushambuliaji kwa kupachika mabao michezo mbalimbali.

Kuhusiana na safu wa ulinzi pluijm amesema kwa wachezaji waliobaki katika kikosi chake kipya alichokitengeneza amebaini wana mapungufu madogo madogo ambayo amesema atayafanyia kazi kabla ya michezo ya Ligi haijaanza ili kujenga usawa wa vikosi viwili ambavyo vitakuwa vikisaidiana.

"Katika michezo yote miwili tuliyoruhusu bao sisi ndio tumeanza kufungwa sababu kubwa ni mabeki kushindwa kuelewana na wamekuwa wakitegeana, mabao yote yaliyofungwa makosa ni ya mabeki lakini nimekaa na wachezaji wote na kuwaambia makosa yao na nini wakirekebishe naamini nitakuwa na vikosi viwili bora vitanisaidia sana," alisema Pluijm.