Simba, Yanga kutamba Ligi Kuu

HUENDA klabu za Simba, Azam  na Yanga zikaendelea kutamba katika Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na kukosekana kwa mdhamini mpaka Agosti 22 wiki ijayo ambapo itaanza. 

Mtendaji mkuu wa bodi ya Ligi, Boniface Wambura amesema ligi itaanza kama ilivyopangwa na watakuja kuwatangaza wadhamini wakati ikiwa inaendelea. 

Wambura alisema wapo katika mazungumzo na makampuni mengi ambayo kati ya hayo mdhamini wa msimu uliopita Kampuni ya Mtandao ya Vodacom ni miongoni mwao. 

Anasema sababu ambayo imepelekea kutuingia mkataba mpya haraka na vodacom ni kutaka baadhi ya mambo muhimu ambayo yalikuwa katika mkataba wa awali yaboreshwe kwanza. 

"Ukiangalia awali Vodacom walikuwa wanatoa jezi pea mbili nyumbani na ugenini na vifaa vingine kama viatu na vingine lakini msimu huo kulikuwa na timu 16 na vifaa vilikuwa havitoshelezi kwa kila timu ndio maana tunataka kama tukisaini mkataba mpya timu zifaidike zaidi ya hapo. 

"Maamuzi ya kuongeza timu tulishirikiana na klabu zote za Ligi Kuu na tulikubalina lakini hata hii si sababu ya kuchelewa kupata mdhamini bali tunataka ambaye tutasaini nae mkataba aweze kutoa zaidi ya vile ambavyo tulikuwa tukipata katika mkataba wa awali. 

"Baada ya kuona changamoto hiyo na Vodacom ambao tupo nao katika mazungumzo tunaongea pia na makampuni mengine kama wanaweza kutupatia zaidi ya hivyo kwani wao kuna faida kubwa wanaipata kama wakiwa wadhamini wakuu, " alisema. 

"Kwahiyo tunaendelea na mazungumzo ambayo kama tutafikia muafaka na kampuni ambayo itatoa vitu ambavyo vinakazi mahitaji muhimu ya kila timu tutasaini mkataba mpya na kumtangaza kama mdhamini mkuu lakini sasa tutabaki na wadhamini wenza waliokuwepo, " alisema Wambura. 

"Kuhusu ili la udhamini kuchelewa tumeshaongea na viongozi wa klabu zote za Ligi Kuu na tumesha kubaliana kutumia vifaa vyao kwanza ambavyo wamekiri wanaweza kujimudu mpaka hapo pesa ya mdhamini mkuu atakapoingia, " aliongezea Wambura. 

Kama Ligi itaanza bila ya kuwa na pesa ya udhamini kama Wambura alivyosema klabu za Simba, Azam na Yanga ambazo zinauwezo wa kujiendesha zitaendelea kutamba.

Wambura alisema msimu ujao katika kuingia uwanjani wanatangaza tiketi kwa nusu bei kwa wanafunzi wote wa sekondari na shule ya msingi ambao watatambulika kwa vitambulisho vyao. 

"Tiketi hizi zitakuwa nusu bei kwa hile pesa ambayo wataingia watu wazima uwanjani lakini pia watakaa maeneo yale ya viti vya kawaida na si viti maalumu na kama kuna ambaye atataka mwanae au mwenyewe kukaa hapo anatakiwa kuwa na tiketi ya eneo hilo, " alisema Wambura. 

Nae Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Mario Ndimbo alitangaza waamuzi Elly Sasii ambaye atachezesha wasaidizi ni Frednand Chacha, Helen Mduma na Jonisya Rukya atakuwa mwamuzi wa akiba watachezesha mechi ya fainali ya Ngao ya hisani.