Simba, Yanga kazi imeanza

Muktasari:

  • Hali ikiwa hivyo watani zao Simba ambayo juzi usiku waliifumua African Lyon kwa mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa Azam Complex, Chamazi itaendelea na mazoezi kujiandaa na mashindano manne wanayokabiliwa nayo, huku kocha wake, Joseph Omog akiungana na nyota wake hao jijini Dar es Salaam.

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina akitarajiwa kutua nchini kesho, vijana wake leo Jumapili watashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuvaana na Polisi Tanzania, ikiwa ni mechi ya kutesti mitambo kujiwinda na Ligi Kuu Bara.

Hali ikiwa hivyo watani zao Simba ambayo juzi usiku waliifumua African Lyon kwa mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa Azam Complex, Chamazi itaendelea na mazoezi kujiandaa na mashindano manne wanayokabiliwa nayo, huku kocha wake, Joseph Omog akiungana na nyota wake hao jijini Dar es Salaam.

Omog aliyekuwa Cameroon kwa mapumziko, ataanza kibarua chake kesho kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, wakati Shirikisho la Soka nchini, (TFF) likianika mechi za raundi ya 12 zitapigwa kati ya Desemba 29 na Januari 1.

Ligi ilisimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika nchini Kenya na inayohitimishwa leo mjini Machakos kwa mechi ya fainali kati ya Zanzibar na Kenya, lakini Simba na Yanga na klabu nyingine za Ligi Kuu zilikuwa zikijifua na huku zikiendelea na usajili wa dirisha dogo.

Yanga na Simba zinatarajiwa mashindano manne ya Ligi Kuu, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi na michuano ya kimataifa na kuanzia leo zitakuwa katika mawindo ili kuhakikisha hakuna kinachowapita katika michuano hiyo.