Simba yajificha Zbar, Yanga Moro

Muktasari:

  • Klabu hizo kongwe zimekuwa na utamaduni wa kuweka kambi nje ya Dar es Salaam kila inapokaribia mechi baina yao.

Dar es Salaam. Homa ya mechi ya watani wa jadi imepanda. Simba inaondoka Dar es Salaam leo Jumatatu kwenda Zanzibar kuweka kambi lakini wenzao Yanga wanatokea Shinyanga kuelekea Morogoro.

Simba na Yanga ambazo zinacheza Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, zimeanza harakati za kuwindana kila mmoja akijiweka sawa kwa pambano hilo ambalo ni turufu muhimu kwa ubingwa.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema; "Tuna mechi ngumu  dhidi ya Yanga, tutaondoka wote kuelekea Zanzibar katika kambi ya pambano la watani," alisema.

Mara ya mwisho Watani hao walikutana katika mechi ya Ngao ya Hisani ambapo Simba ilitokea Unguja na Yanga kisiwa cha Pemba na Simba kuibuka na ushindi wa penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana.

Habari za uhakika kutoka Shinyanga zinasema kwamba Yanga safari hii haitakwenda Zanzibar bali itakwenda kutulia Morogoro mpaka siku moja kabla ya mechi ya watani ambayo ni Ijumaa.