Siku 20 za presha kwa wagombea

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) bado ni mbichi kwa wagombea wanaowania nafasi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 12, mjini Dodoma kwa sasa wameingia kwenye kipindi cha siku 20 za presha.

Wagombea hao watalazimika kupita katika hatua saba ndani ya siku hizo, ngumu na muhimu ili waweze kujihakikishia nafasi ya kuingia hatua mbili za mwisho zinazosubiriwa kwa hamu ambazo ni kipindi cha kampeni kwa wagombea sambamba na zoezi la kupiga kura kwa wajumbe wa mkutano mkuu.

Hatua ya kwanza katika hizo saba ambazo wagombea watapaswa kupitia ni ile ya usikilizaji wa rufaa za kimaadili ambayo kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, imefanyika kwa siku nne kuanzia Julai 18 hadi leo Jumamosi kabla ya kutolewa uamuzi wa rufaa za kimaadili kati ya kesho Jumapili na Julai 25.

Hatua ya tatu ambayo wagombea hao watapitia ni ukataji rufaa dhidi ya kamati ya uchaguzi kwa kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, iliyopangwa kufanyika kati ya Julai 26 hadi 28.

Kuanzia Julai 29 hadi Agosti 2, ni kipindi cha kusikiliza rufaa zilizokatwa mbele ya kamati ya rufaa ya uchaguzi wakati kuanzia Agosti 3 hadi 4 ni kipindi cha kuwajulisha wagombea na kamati ya uchaguzi, uamuzi uliotolewa na kamati ya rufaa ya uchaguzi na baada ya hapo, zoezi la kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea itachapishwa na kutangazwa kuanzia Agosti 5 hadi 6 mwaka huu.

Hatua ambazo kidogo zinaonekana hazitokuwa na presha kwa wagombea ni hatua ya kampeni ambayo itaanzia Agosti 7 hadi 11 na uchaguzi wenyewe utakaofanyika Agosti 12.