Shiza Kichuya, Ajibu wapewa mchongo

NYOTA wa soka wa klabu za Simba na Yanga na klabu nyingine nchini akiwamo Shiza Kichuya na Ibrahim Ajibu wamepewa mchongo na nyota wa zamani wa Liverpool Sami Hyypia aliyesisitiza kama wakikaza kidogo tu wanatoboa kimataifa.

Gwiji huyo aliyetua nchini akijiandaa kuzindua mashindano ya Standard Chartered, alisema kuwa wachezaji wenye vipaji wa Afrika na Tanzania wana fursa kubwa kucheza soka la kulipwa England na pia nchi nyingine endapo tu wataongeza bidii.

Hyypia alisema tangu enzi za Tony Yeboah ambaye alicheza naye, kwa sasa Afrika kuna nyota kama Sadio Mane, Mohamed Salah na wengine wengi wanaotamba katika ligi mbalimbali barani Ulaya na mabara mengine.

Alisema atafanya mazungumzo na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kupitia benki iliyomleta ili kuona wanafanya jitihada gani ili kuwawezesha wachezaji wa Tanzania kucheza soka nje.

“Bahati nimekutana na viongozi wa TFF hasa Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, pia nitakutana na Waziri wa Michezo, nini kitafanyika, naomba msubiri,” alisema Hyypia.

Awali, Mkurugenzi wa benki hiyo, Sanjay Rughani alisema wamefarijika kwa ujio wa Hyypia na mbali ya kuzindua mashindano Standard Chartered Cup Jumamosi, pia atakutana na watoto wa wateja wa benki hiyo na mashabiki wa timu wa Liverpool.

Rughani alisema Hyypia pia atakutana na wachezaji 224 kutoka timu 32 zitakazoshiriki katika mashindano ya mwaka huu ambapo mshindi ataenda Liverpool, Septemba mwaka huu.