Shinyanga, Magu zaanga kwa kishindo

Mwanza. Timu za Shinyanga, Magu na Nyuki zimeanza vyema mashindano ya mpira wa Wavu (Mirjam Championship) baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zao za awali.

Mashindano hayo yameanza kurindima leo katika kituo cha michezo, Mirongo yanashirikisha timu nane kutoka Mikoa mitano ya Tanzania Bara na Visiwani na yatafikia tamati Machi 25 mwaka huu.

Katika michezo hiyo, Nyuki ya Zanzibar imeinyuka Bunda ya mkoani Mara seti 3-2, Shinyanga ikaifumua SAUT seti 3-2 na Magu ya Mwanza ikailaza Ngorongoro ya mkoani Arusha seti 3-0.

Mratibu wa mashindano hayo, Majaliwa Mayunga amesema walitarajia timu za mikoa yote ya Tanzania na visiwani kushiriki, lakini ni mikoa mitano pekee ambayo imejitokeza na kwa kuwa ni mara ya kwanza wanamini mwakani watajitokeza zaidi.

Kuhusu zawadi alisema kamati imejipanga vizuri na kila kitu kipo sawa.

Mikoa inayoshiriki ni Mwanza yenye timu tatu za Magu, SAUT na MTC, Mara yenye timu ya moja ya Bunda, Zanzibar yenye timu mbili za Polisi na Nyuki, Arusha yenye timu moja ya Ngorongoro na Shinyanga iliyowakilishwa na SVC.