VIDEO: Shilole afikia jikoni msiba wa Masogange

Muktasari:

Agnes ‘Masogange’ anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao

Mbalizi, Mbeya. Mwanamuziki Shilole ni miongoni mwa wasanii waliofikia alfajili ya leo nyumbani kwa marehemu Agnes Gerald 'Masogange' Mtaa wa Utengule, Mbalizi moja kwa moja aliingia jikoni kuanza kuandaa chakula kwa ajili ya wageni.

Agnes ‘Masogange’ anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao na baadhi ya wasanii wameingia alfajiri ya leo Mbeya kwa ajili ya kumsindikiza mwenzao.

Mwili wa marehemu bado haujafika na waombolezaji wanazidi kumiminika msibani nyumbani hapo.

Shilole alipofika alionekana kuchangamka kuingia jikioni na kusaidiana na wenyeji katika kuandaa vyakula kwa ajili ya wageni.

Mapema jana baba mzazi wa Agnes Masogange anayeitwa,  Gerald Waya amesema, mwanaye alikuwa nguzo katika maisha yao na kifo chake ni pigo kubwa kwake na familia kwa ujumla.

Waya amezungumza na MCL Digital nyumbani kwake alisema Masogange ni mtoto wanne katika familia yake ya watoto sita ambapo wakike ni watano.

Alisema, Masogange amesoma Shule ya Msingi Utengule-Mbalizi na Sekondari ya Sangu akaishia kidato cha pili.

Waya alisema Masogange alipata matatizo hivyo akalazimika kuacha shule. Hata hivyo amesema hataki kuzungumzia mambo mabaya wakati huu anapoomboleza kifo cha mwanaye.

“Aliishia form two (kidato cha pili), akapata matatizo ikabidi aache shule. Tulikosana kidogo, lakini tukayamaliza yeye akaenda Dar es Salaam.”

Waya alisema, “Mwanangu alikuwa nguvu kwangu, alikarabati nyumba hii ninayoishi kwa sasa na nilikuwa nafarijika sana, lakini leo kusikia msiba huu kwa kweli inaniuma sana.”

Alisema Masogange alimpigia simu, “Tukaongea naye akaniambia ‘mimi baba ninaumwa’.Nikamuuliza nini tatizo akasema, “aah!   baba niombee tu kwa Mungu’. Na Jumamosi iliyopita nilimpigia simu wakati yupo hospitali kujua maendeleo yake lakini akaniambia ‘baba byee’. Nikaanza kulia, na hapo sikuwasiliana naye tena hadi nilipopata taarifa za kifo chake,”alisema Waya.