Shilole adai Uchebe anaitwa baba, wengine uncle

Dar es Salaam.Mwanamuziki wa Bongo fleva,Shilole amesema kati ya wanaume aliokuwa nao katika mahusiano, ni Ashirafu Uchebe peke yake ndio watoto wake wamekubali kumuita baba huku engine waliishia kuitwa ‘uncle’.

Desemba mwaka jana Shilole ambaye jina lake halisi ni Zuwena Mohamed na Ashirafu Uchebe  walifunga ndoa, iliyofuatiwa na sherehe ya kukata na shoka iliyofanyika Januari 15 na kuhudhuriwa na mastaa mbalimbali nchini akiwemo Diamond ambaye huwa ni nadra kuonekana kwenye matukio ya aina hiyo.

Wakati listi ya wanaume ambao amewahi kutoka nao kabla ya ndoa hiyo ni pamoja na Nuhu Mziwanda waliyeteka vichwa vya habari kila uchwao kutokana na visa na mikasa isiyowaisha.

Pia, inaelezwa wengine iliowahi kubanjuka nao kwa nyakati tofauti  ni  Boy Caro, Ney Music, Barnaba na Timbulo.

Pamoja na listi hiyo ya wanaume, Shilole amebainisha kwamba watoto wake Joyce na Rahma hawajawahi kuwaita baba zaidi ya kuambulia kuitwa Uncle isipokuwa Uchebe.

Shilole alisema kupendwa huko kwa Uchebe hadi kuitwa baba anadhani wameona mama yao kapata mume bora na anayeweza kusaidiana naye katika kuwalea.

“Huwezi amini katika wanaume wangu wote, Uchebe amepokelewa kitofauti sana na watoto wangu mpaka wamekubali kumuita baba wakati wengine walikuwa wakiishia kuitwa ‘Uncle’.

“Nadhani pia wamemuona mama kapata mtu wa kusaidiana naye na huwa wanampenda zaidi na kumsikiliza kuliko mimi, kwa kweli nashukuru kwa hilo,”alisema.

Akizungumzia tuhuma za kuwa amekuwa amekuwa akimlea kama mtoto wake, Msanii huyo alikanusha jambo hilo na kueleza kuwa hata yeye ana kazi anafanya na amekuwa na mchango katika familia ikiwemo kumwachia hela ya kula kila siku.

Wakati kuhusu suala la kumpelekesha, alisema hilo halina ukweli kwani ni mtu ambaye anamsimamo yake na huwezi kumpanda kichwani katika jambo ambalo analiamini yupo sahihi.