Shearer amchongea Lukaku

Muktasari:

Mshambuliaji huyo alipoteza nafasi za kufunga na kutegeneza mabao dhidi ya Man City

London, England. Nahodha wa zamani wa Newcastle United na England, Alan Shearer amemponda mshambuliaji wa Manchester United, Romelu Lukaku.

Shearer alisema Lukaku ameshindwa kuonyesha thamani ya Pauni 75 milioni aliyonunuliwa katika usajili wa majira ya kiangazi kutoka Everton msimu uliopita.

Kauli ya mshambuliaji huyo wa zamani, imekuja muda mfupi baada ya Man United kuchapwa mabao 2-1 na Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa juzi usiku Old Trafford.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, alianza vyema Man  United kabla ya kupoteza mwelekeo na kuanza kuibua maswali mengi kuhusu ubora wake uwanjani.

 

Lukaku amefunga mabao manane msimu huu katiika Ligi Kuu England kati ya Agosti na Oktoba, bao la mwisho alifunga mwezi uliopita katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Newcastle United.

Nguli huyo ambaye ni kocha na mchambuizi wa soka, alidokeza mchezaji huyo alicheza chini ya kiwango mchezo wa juzi usiku na hakuwa na madhara langoni mwa Man City.

“Hakuna mtu aliyehoji maswali haya baada ya Lukaku kufunga mabao 11 katika mechi 10 mapema msimu huu. Amepoteza hali ya kujiamini,” alisema Shearer.

Alisema mshambuliaji wa kati anatakiwa kuwa makini langoni mwa adui na kazi yake kubwa ni kufunga mabao, anapopata nafasi lazima atumie.

“Najua atakuwa katika hali gani, hata mimi nilipokuwa sifungi nilikuwa sipati usingizi kwa siku tatu au nne hadi nifunge bao ndio natulia,”alisema Shearer.