Serikali kujibu hoja ya kuifuta kesi ya Aveva Sept 18

Muktasari:

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000

Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili waliokuwa viongozi wa Klabu ya Simba, umepanga Septemba 18, mwaka huu kuwasilisha majibu dhidi ya hoja iliyowasilishwa na upande wa utetezi ya kutaka mahakama iwafutie mashtaka, washtakiwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, ambao wanakabiliwa na mashtaka 10, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai leo Septemba 14, 2018, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka ulitakiwa leo kuwasilisha majibu dhidi ya maombi yaliyotolewa na upande wa utetezi ya kutaka  mahakama hii iwafutie mashtaka Aveva na Nyange, lakini kwa bahati mbaya, Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai, amepata udhuru na hivyo ameshindwa kufika mahakamana" alidai Kishenyi na kuongea.

"Hivyo kutokana na hali hiyo, tunaomba mahakama ipange tarehe fupi kwa ajili ya kuja kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi " alidai Kishenyi.

Kishenyi baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, mwaka huu itakapotajwa.

Septemba 7, mwaka huu, upande wa utetezi uliomba Mahakama hiyo iwafutie mashtaka, washtakiwa hao kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kuiendesha kesi.

Maombi hayo yaliwasilishwa na Wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko, baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama kuwa DPP bado hajalipitia jalada la kesi hiyo, kutokana na kuwa katika harakati za kuanzisha Ofisi mpya mkoani Dodoma.

Hata hivyo, Julai 17, Mwaka huu, Mahakama hiyo, ilitoa siku saba kwa upande wa mashtaka kubadilisha hati ya mashtaka katika kesi.

Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Wanadiawa, kuwa Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.