Serikali, wasanii kujadili upya tozo za Basata

Muktasari:

Waziri Mwakyembe amesema amewapa nafasi wasanii wakajadili kwa upana na kisha kumletea mapendekezo yao wangetaka fedha hiyo itoleweje.

Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Serikali imefungua milango kwa wasanii kujadili suala la tozo ya Sh5 milioni na makampuni tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao kati ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kilicholenga kusikiliza nini wangependa kiboreshwe katika kanuni hizo mpya zilizotolewa hivi karibuni na Baraza lA Sanaa la Taifa(Basata).

Waziri Mwakyembe amesema amewapa nafasi wasanii wakajadili kwa upana na kisha kumletea mapendekezo yao wangetaka fedha hiyo itoleweje.

Baadhi ya wasanii akiwemo Katibu Mkuu wa chama cha Wasanii wa muziki wa kizazi kipya(Tuma), Samuel Mbwana 'Braton' amesema wangependa asilimia ya fedha ambayo msanii analipwa katika mikataba hiyo ndio iingizwe kwenye mfuko kwa kuwa siyo wote wanaopata kazi za kulipwa Sh5 milioni.

"Mfano msanii umepata kazi ya shilingi laki mbili, basi tutakubaliana kati ya hizo kampuni ipeleke asilimia ngapi kati ya hizo, badala ya kumwambia atue milioni tano kwa mkupuo."

Naye msanii Ditto amesema kitendo cha serikali kutenga muda wa kuwasikiliza wasanii kimemkosha kwani malalamiko yalikuwa mengi mtaani kiasi cha wasanii kufika hatua ya kuichukia kazi hiyo ya sanaa.