Serengeti inatoa tu mkwanja

Friday January 12 2018

 

By THOMAS NG’ITU

LICHA ya awali kuwekeza ndani ya Taifa Stars kwa udhamini mnono wa Sh2.1 bilioni kwa mkataba wa miaka mitatu, Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL), imeongeza udhamini wake katika soka la Bongo.

Kampuni hiyo inayotengeneza bia za Serengeti Lager, Serengeti Lite na Tusker, imeimwagia mamilioni Ligi ya Wanawake na kufanya sasa ishike namba tano katika orodha ya kampuni zinazotoa fedha nyingi kwenye soka nchini.

Kupitia bia yake ya Serengeti Lite, kampuni hiyo imetoa kiasi cha Sh450 milioni kudhamini Ligi ya Wanawake itayaoingia hatua ya nane bora baadaye mwezi ujao. 

Kwa nyongeza hiyo ya udhamini wake, sasa inazidiwa na kampuni za Azam TV, SportPesa na Vodacom ambazo ndizo zinamwaga mkwanja mnene zaidi kwenye soka la Bongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Helene Weesie,  alisema wameingia mkataba wa kuidhamini ligi hiyo ili kuongeza mvuto wake pamoja na kusaidia kunyanya soka hilo la wanawake ambalo bado lipo chini.